Tuesday, November 12, 2024

Uwekezaji wa iTrust Finance utasaidia upatikanaji wa fedha za miradi


KAMPUNI ya iTrust Finance imezindua mfuko wa uwekezaji wa pamoja wenye lengo la kutoa fursa kwa wawekezaji wengi kuwekeza katika dhamana mbalimbali ikiwa ni moja ya utekelezaji wa mikakati ya serikali kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za fedha kwa wanachi wengi vijijini na mijini.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango wa uwekezaji wa pamoja wa kampuni ya iTrust Fiance Limited unaojumuisha mifuko mitano pamoja Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama amesema Mfuko huo unalenga kuwawezesha wawekezaji wadogo na wakubwa kushiriki katika masoko ya fedha na mitaji.

"Kuanzishwa kwa mifuko hii ni hatua muhimu katika juhudi za serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi kote nchini, ikiwa ni pamoja na vijijini ili kuwasaidia kiuchumi.

Mifuko hiyo ni ya iCash (mfuko wa soko la fedha), iGrowth(mfuko wa uwiano), iIncome(mfuko wa mgao wa mapato), iSave(mfuko wa mapato ya kudumu) na imaan(mfuko wa unaozingatia misingi ya shariah) Kila mfuko una lengo tofauti kulingana na mahitaji ya wawekezaji, kama vile kuimarisha mtaji, kupata mapato au kuweka akiba.

Amesema kuwa utekelezaji wa azma hiyo umeainishwa katika mpango wa tatu wa huduma za fedha wenye lengo kuongeza ushiriki wa wanachi kwenye sekta rasmi ya fedha ikiwa ni pamoja na masoko ya mitaji.

Mukama amesema mamlaka hiyo iliidhinisha nyaraka za matarajio (offer documents) na mikataba ya uendeshaji wa mifuko mitano ya uwekezaji wa pamoja ya makampuni iTrust Finance Limited Oktoba 11 20224 na kwamba idhini ilitolewa baada ya kukidhi matakwa ya sharia ya masoko ya mtaji na dhamana sura ya 79 na kanuni ya Masoko ya mitaji na dhamana sura ya 79 ya sharia za Tanzania.

Amesema mauzo ya awali ya vipande vya uwekezaji katika mifuko hii yalianza Novemba 12, 2024, na kampuni inatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 37 ndani ya mwezi mmoja.

"Uwekezaji katika mifuko hii una manufaa mbalimbali katika ustawi wa jamii na maendeleo ya uchumi hapa chini," amesema Mukama.

Aidha amesema fedha hizo zitawekezwa katika masoko ya fedha na mitaji, ikijumuisha hisa za kampuni zilizoorodheshwa kwenye Soko la Hisa, hatifungani za serikali, hatifungani za kampuni, na dhamana za serikali za muda mfupi.

"Lengo la uwekezaji wa aina hii ni kuifanya mifuko kuwa na ukwasi unaotosha ili kukidhi mahitaji ya fedha za wawekezaji pindi mahitaji yanapotokea. Aidha, kwa upande wa mfuko wa Imaan, fedha zitakazopatikana zitawekezwa kwenye bidhaa za masoko ya mitaji zinazozingatia misingi ya Shariah, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika hatifungani za Sukuk."

"uwekezaji utakaofanywa na Mifuko hii katika hatifungani za Serikali utawezesha upatikanaji wa rasilimali fedha za kugharamia miradi ya maendeleo kama ambavyo ilivyoainishwa katika Mkakati wa Serikali wa njia mbadala za kugharamia miradi ya maendeleo yaani Alternative Project Financing (APF) Strategy."

"wawekezaji watalipwa gawio kutokana na faida za uwekezaji na wakati huo wakiwa ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutokana na fedha za mifuko kuwekezwa katika hatifungani za Serikali." Alisema

Mkama alisema Faida nyingine ya kuwekeza katika Mifuko hii ni kuwa vipande vya uwekezaji vinaweza kutumika kama dhamana ili kuwezesha wawekezaji kupata mikopo kutoka taasisi za fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri, uwekezaji nchini Tanzania umepiga hatua kubwa.

"Mwaka 2020 TIC ilisajili miradi ya uwekezaji yenye thamani ya takribani dola bilioni 2, lakini hadi kufikia Novemba mwaka huu, thamani ya miradi hiyo imefikia karibu dola bilioni 7, hii hii inajumuisha miradi ya sekta kama viwanda, mashamba makubwa, utalii, uchukuzi, na majengo ya kibiashara, ambayo yamechangia kuongeza ajira na mitaji nchini Tanzania". Amesema

Kuhusu uwekezaji wa masoko ya fedha (iTrust), Teri amesisitiza umuhimu wake, akieleza kuwa ili uwekezaji wa kawaida ukue, ni lazima kuwe na fedha za kutosha kwenye uchumi. Uwekezaji huu wa iTrust unaleta fedha muhimu zinazosaidia ukuaji wa uchumi.

Naye, Nalitolea Peter, Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam, amesema uzinduzi wa mifuko hiyo ni njia mojawapo ya taasisi za kifedha kama iTrust kuweza kupanua wigo wake katika uwekezaji kwenye soko la hisa

"Taasisi za kifedha zitakapowekeza huwa ni nguvu ya kuanzisha soko, kuongeza ukwasi na kukuza mtaji, Kwa hiyo taasisi hizi huwa zinakuwa na nguvu kubwa ya kuweza kuwekeza na hivyo kuweza kufanya ununuaji na uuzaji wa hisa urahisishwe zaidi"

Amesema masoko ya mitaji na dhamana yakiendelea kukua na soko la hisa limekua hadi kufikia juzi jumla ya thamani ya mitaji katika soko la Hisa imefika shilingi Trilioni 18.5

"Mafanikio haya ni jambo jema kwa watanzania kwani wawekezaji ambao wamewekeza katika Masoko ya mitaji na dhamana wanapata faida hata kwenye uwekezaji wao na thamani ya uwekezaji wao kupanda lakini pia ni faida kwa serikali"

Mjumbe wa Bodi ya iTrust Finance Limited, Prof. Mohamed Warsame, amewataka Watanzania kuwekeza katika mifuko hiyo mitano ya iTrust kwani inaleta faida kubwa kwa wawekezaji na kuchangia katika maendeleo ya kifedha nchini.



 

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...