Tuesday, November 12, 2024

CAMFED TANZANIA YASAIDIA WASICHANA 500,900 ELIMU SEKONDARI


SHIRIKA lisilo la kiserikali la ufadhili wa masomo kwa watoto wa kike wanaoishi katika mazingira magumu (CAMFED Tanzania) limesema kuwa hadi sasa limeshawasaidia wasichana 500,900 kupata Elimu ya Sekondari.

Hayo yamesemwa leo Novemba 11, 2024 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Miradi na Ushirikiano kutoka Camfed Tanzania, Anna Sawaki katika mkutano Mkuu wa nne wa kimataifa wa kuangalia ubora wa elimu.

Amesema kwa zaidi ya miaka kumi na tano wamekuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana na serikali kuhakikisha kila mtoto wa kike anayetoka katika mazingira magumu anapata Elimu bora.

Amefafanua kuwa, pia wasichana 5,600 wamenufaika kupata Elimu kwa ngazi ya elimu ya juu kuanzia cheti hadi Shahada (degree) kwa kushirikiana na bodi ya Mikopo.

"Kwa kutambua kuwa mtoto wa kike ana sababu nyingi zinazomfanya aache shule, pia tuna miradi mingine ambayo inamuwezesha anapokuwa shuleni kusoma na kufaulu vizuri.

"Miradi hiyo ni ya stadi za maisha kama ambavyo tumesikia wizara inasema inasaidia umuhimu WA elimu hiyo shuleni," amesema na kuongeza:

"Kwahiyo kupitia wasichana ambao tumewasapoti na wao wanarudi mashuleni kwaajili ya kutoa ushauri (mentorship) na stadi za maisha kwa wanafunzi wawapo shuleni na kwenye jamii kwa kuangalia watoto ambao Wana dalili za kuacha shule na kuwasaidia ili waweze kubaki shule,".

Akizungumzia kuhusu ushiriki wao kwenye mkutano huo, amesema wao ni miongoni mwa wananchama wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet) na wako hapo kuhakikisha kunakuwa na mfumo ambao utamnufaisha mtoto kama ambavyo sera inasema bila kuangalia anatoka kwenye mazingira gani.

"Kwahiyo tupo kushirikiana na wadau wengine ambao tuna kampeni kwaajili ya elimu bora kwa watoto wote," amesisisitiza.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...