Na John Walter -Manyara
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Cuthbert Sendiga amewataka wakandarasi watakaotekeleza miradi ya Maji katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko ya tope wilayani Hanang kutekeleza miradi hiyo kwa muda uliopangwa, kwa ubora unaotakiwa na kuishirikisha jamii ambao ndio wanufaika wa mradi.
Ameyasema hayo leo Septembea 2, 2024 katika hafla fupi ya utiaji saini mikataba ya utekelezaji wa miradi miwili ya maji kati ya RUWASA na Wakandarasi watakaofanya kazi ya usambazaji maji kwenye makazi mapya ya waathiriwa wa maporomoko wilayani Hanang'.
Miradi hiyo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.7 imepangwa kunufaisha zaidi ya Vijiji 5 ambavyo vilivyoathiriwa na mafuriko yaliyotokea mwezi Desemba mwaka jana wilayani humo.
Aidha Sendiga amemshukuru Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa zaidi ya Bilioni 9.4 kwa ajili kuendelea kuwezesha urejeshwaji wa miundombinu na huduma za maji wilayani Hanang'.