Na Anangisye Mwateba- Bariadi Simiyu
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) leo tarehe 12 Septemba 2024 amepokea majengo 9 kutoka Halmashauri ya Bariadi ili yatumike kuendeshea mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi watakaokuwa wanasoma kozi za usimamizi wa wanyamapori na waongoza watalii kupitia Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi.
Majengo hayo ambayo awali yalikusudiwa kutumika kama sekondari ya wasichana yamejengwa katika eneo linalokabiliwa na changamoto ya uvamizi wa tembo; hivyo ili kuepusha athari hiyo kwa wanafunzi wa kike, na vilevile kufuatia kujengwa kwa shule mpya ya wasichana katika wilaya ya Bariadi; serikali ya mkoa wa Simiyu ilifikia maamuzi ya kutoa majengo ya shule tarajali ya wasichana Matongo kwa wizara ya maliasili na utalii ili yatumike kama taasisi ya kutoa mafunzo ya uhifadhi wa maliasili nchini.
Katika hotuba yake Naibu Waziri Kitandula alisema kuwa kutumika kwa eneo hilo lililopo kata ya Giliya kuendeshea mafunzo ya vitendo kupitia Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi kutatoa fursa ya kiulinzi katika eneo husika na maeneo inayopakana nayo, hivyo kuwahakikishia ulinzi wananchi waliokuwa wanavamiwa na wanyama wakali na waharibifu mara kwa mara, na wakati mwingine wanyama hao kusababisha vifo.
Mhe. Kitandula aliongeza kuwa uwepo wa Chuo cha Taaluma ya Uhifadhi wa maliasili katika wilaya ya Bariadi pia kutatoa fursa kwa jamii kujifunza na kutumia mbinu za kuzuia wanyama wakali na waharibifu
Aidha, Mhe. Kitandula alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wataalam wa halmashauri zote nchini kuacha tabia ya kuanzisha shughuli za kijamii kwenye maeneo ya mapito ya wanyama (shoroba) au karibu na hifadhi za taifa au mapori ya akiba. Mhe. Kitandula asisisitiza kuwa nilazima wakati wote uanzishwaji wa shughuli za maendeleo uzingatie mipango ya matumizi bora ya ardhi.
Awali akimkaribisha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe. Simon Simalenga akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu alisema moja ya Mipango ya Mkoa wa Simiyu ni kujenga uwanja wa Ndege ambao utatumika kuleta watalii wa Nje na ndani hivyo kuchochea mapato yangiayo kupitia uhifadhi na utalii.
Shule ya sekondari ya Wasichana-Matongo ilianza kujengwa tangu enzi za awamu ya nne. Shule hii pamoja na kukamilika haikuwahi kudahili wanafunzi kutokana na kuwepo kwa changamoto ya Wanyamapori wakali na waharibifu kama tembo ambao mara kwa mara wamekuwa wakivamia eneo husika na kusababisha madhara kwa wakazi wa maeneo hayo na wakati mwingine kusababisha vifo.