Friday, August 16, 2024

Waziri wa fedha kuweka jiwe la msingi ujenzi wa chuo cha Uhasibu kampasi ya Babati.

Na John Walter -Babati 

Waziri wa fedha Dkt Mwigulu Nchemba anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika chuo cha Uhasibu Arusha tawi la Babati mkoani Manyara kuweka jiwe la msingi ujenzi wa chuo hicho awamu ya kwanza.

Taarifa iliyotolewa na Meneja wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kampasi ya Babati, Dr Eliakira Nnko, Dkt Nchemba anatarajiwa kufika chuoni hapo Agosti 22,2024.

Akieleza kuhusu ujenzi wa chuo hicho, Dr Nnko amesema majengo ya hosteli yamefikia asilimia 75 ya ujenzi wake na gharama yake ni shilingi  Bilioni 4.

Jengo la taaluma na ofisi za Wanafunzi ambalo lipo katika hatua za mwisho za umaliziaji gharama yake ya Ujenzi ni shilingi bilioni 5, bwalo la chakula shilingi bilioni 1 na kwa sasa limefika asilimia 45 ya ujenzi.

Dr Nnko ameeleza kuwa ujenzi wa majengo hayo wanatumia mfumo wa malipo wa Force account kupitia mafundi wa kawaida ambao hutumia gharama ndogo ukilinganisha na kutumia wakandarasi.


Amesema Wanafunzi wanatarajiwa kuanza kuingia chuoni hapo kuanzia Mwezi wa 10, 2024 mwaka wa masomo unapoanza. 

Aidha chuo hicho kina uwezo wa kupokea Wanafunzi 2500 hadi 2700.

Mkuu wa mkoa wa Manyara Mheshimiwa Queen Sendiga amefika chuoni hapo kuangalia maandalizi ya mapokezi ya mgeni huyo wa kitaifa akiwapongeza kwa usimamizi wa ujenzi wa awamu ya kwanza.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...