Na Ahmad Mmow, Lindi.
Katika kuhakikisha kunakuwa na kumbukumbu sahihi za kazi na shughuli zinazofanywa na wawekezaji wa ndani. Wametakiwa kusajili kazi na shughuli wanazofanya kwa mujibu wa sheria.
Wito huo ulitolewa jana mjini Lindi, na mkuu wa wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga wakati wa semina ya uhamasishaji uwekezaji wa ndani iliyoandaliwa na kituo cha uwekezaji nchini(TIC).
Ndemanga alitoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji kusajili kazi na shughuli zao za kiuchumi ili zitqtambulike na serikali. Kwani wataweza kuzijua na kupata fursa mbalimbali.
Ndemanga ambae katika semina hiyo alimuwakikisha mkuu wa mkoa wa Lindi na kuyashirikisha makundi mbalimbali ya wafanyabiashara, wawekezaji wadogo, taasisi za serikali, taasisi za fedha na waandishi wa habari alisisitiza kuwa ni muhimu Kwa wananchi, hasa wazawa wakiwamo wa mkoa wa Lindi kuwekeza zaidi katika miji yao ili wasaidie upatikanaji wa ajira kwa vijana wazawa. Huku akibainisha kwamba ni vigumu kwa wawekezaji wa nje kutoa kipaumbele cha kuajiri wazawa badala yake fursa zinapelekwa Kwa raia wa nchi zao.
Kwa upande wake ofisa uhamasishaji wa kituo cha uwekezaji Tanzania, Felix John, alifafanua kwamba umuhimu wa kupata usajili wa biashara kutoka katika Kituo hicho ikiwa ni pamoja na kuwa na takwimu sahihi zinazosaidia kutoa taarifa katika mamlaka mbalimbali zinazohusika na sekta ya biashara na uwekezaji. Lengo likiwa ni kusaidia kuratibu mipango endelevu ya kiuchumi.
TIC imeendesha semina ya uhamasishaji uwekezaji wa ndani kwa wafanyabiashara ikiwa ni awamu ya pili baada ya kuzindua Septemba 25, mwaka jana 2023.