Sunday, August 1, 2021

Wanafunzi 12 mkoani Njombe wafanya vizuri kwenye utafiti sasa kushindanishwa Dar


Na Amiri Kilagalila,Njombe.

Wanafunzi 12 kwa mara ya kwanza kutoka shule tofauti mkoani Njombe wamefanikiwa kufanya vizuri kwenye maonesho ya wanasayansi chipukizi (Young Scientists Tanzania) kwa kuandaa utafiti (Reserch) mzuri hatua inayowawezesha wanafunzi hao kujiandaa vizuri ili kushiriki maonesho katika hatua nyigine yanayotarajiwa kufanyika jijini Dar Es Salaam. 

Akizungumza mara baada ya kuwavisha medali pamoja na vyeti ,Mwalimu Charles John ambaye ni afisa taaluma mkoa wa Njombe amesema program hiyo imefanyika kwa mara ya kwanza katika mkoa wa Njombe lakini wanafunzi wamefanikiwa kuonesha vizuri maandalizi yao mazuri ya utafiti katika mazingira yao.

"Watoto wameandaa vitu vizuri na ninajua mbele ya safari katika maonesho mengeni watakayokwenda kuonesha Dar es Salaam wana nafasi nzuri sana ya kuonyesha uwezo wao walio nao.Na nimewakumbusha kuwa watakaoshinda kwenye maonyesho ya kitaifa watapata nafasi ya scholarship kutoka kwenye shirika kwa ajili ya kwenda kusoma chuo kikuu chochote ndani ya nchi au nje ya nchi"alisema Mwalimu Charles John

Fadhil Mwasomola ni mratibu wa Young Scientist mkoa wa Njombe,amesema anaamini wanasayansi chipukizi waliofanikiwa wataendelea kufanya vizuri kama ambavyo malengo ya shirika hilo kwa wanafunzi kukabiliana na chanagamoto za mazingira tuliyo nayo.

"Kwa kuwa tunawaandaa wanafunzi kuweza kukabiliana na mazingira tuliyo nayo kwa hiyo tunaamini kulingana na tafiti wanazozifanya kutona na mazingira yao basi watatusaidia kuibadilisha Tanzania kwa kufanya lolote"alisema Fadhil Mwasomola.

Jesca Mwalongo ni mwanafunzi kutoka shule ya sekondari Hagafilo walioandaa utafiti wa kilimo na Alex Mgimba ni kutoka shule ya sekondari Matola waliondaa utafiti kwenye maswala ya mitandao.Wamesema wamevutiwa kuingia katika mashindano hayo ili kutanua uwezo wao wa kufikiri.

"Niliingia kutokana na uelewa nilioupata ili kujitanua zaidi namna ya kufikiri kutokana na changamoto ambazo tunakutana nazo watanzania"alisema Alex Mgimba

Naye Jesca Mwalongo amesema "Mkoa wetu umekuwa ukikabiliwa na tatizo la utapiamlo kwa hiyo tumeona ni vema kufanya utafiti ili kutatua tatizo la utapiamlo kwa kupata baadhi ya virubisho kutoka kwenye mboga mboga ambazo tunazalisha"

 

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...