Sunday, August 1, 2021

Wachimbaji Wadogo Kupokea Kifuta Jasho Cha Milioni 90 -Singida


Na. Steven Nyamiti – Mkalama Singida
Jumla ya Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu 90 katika eneo la kijiji cha Tumuli wataanza kupokea kifuta jasho kuanzia  tarehe 2 Agosti, 2021 baada ya utaratibu wa kupewa kifuta jasho kukamilika.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Madini Doto Biteko tarehe 31 Julai, 2021 katika kijiji cha Tumuli wilaya ya Mkalama Mkoani Singida wakati wa ziara ya kukagua na kutembelea shughuli za wachimbaji wadogo.

Ameeleza kuwa, wachimbaji watakaopokea kifuta jasho hicho ni wale walioandikishwa na ambao taarifa zao zipo kwenye Kanzidata kufuatia kuondolewa kuchimba kwenye eneo lenye leseni.

"Mgogoro huu una historia ndefu sana zaidi ya miaka 9, mwanzo walikua wachimbaji 26 wanaopaswa kupewa  lakini sasa wameongezeka zaidi ya 100, lazima tutende haki kwa watu wote kuanzia mchimbaji  hadi mwekezaji ili pande zote ziridhike," amesema Biteko.

Aidha, Waziri Biteko ameagiza mgodi wa Chama cha Ushirika cha Uchimbaji Madini (Sekenke One Mining Cooperative Society) uliosimamishwa mwezi Disemba 2019, kutokana na zuio la kiusalama katika mgodi huo ufunguliwe mara moja  ili shughuli za uchimbaji ziendelee.

Biteko amemuagiza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Singida, Chone Lugangizya kuzungumza na kampuni ya Sekenke One ili wakubaliane  waendelee kuchimba dhahabu kwa kuzingatia Sheria na Taratibu.

"Mimi ninachotaka kuona shughuli zinaendelea, utaratibu wa kufunga funga migodi huu huwa hautusaidii sana, tunaopoteza ni sisi, tunachotaka kuona wachimbaji wanarudi kwenye uchimbaji ili masoko haya yaweze kupanuka Zaidi," amesisitiza Biteko.

Kuhusu utatuzi wa mgogoro baina ya Nabii Elia Makuli na kikundi cha Bathlomew Waziri Biteko amerejesha suala hilo kwenye ngazi ya Mkoa na Wilaya kwa ajili ya kulitatua ambapo Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda amehaidi kufanyia kazi mgogoro huo kuanzia siku ya Jumatatu tarehe 2 Agosti.

Naye, Mkuu wa wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo amethibitisha kuwa wilaya yake imepokea fedha hizo kutoka kampuni ya uchimbaji madini ya PuBo (PuBo Mining Limited) kiasi cha Shilingi Milioni 90 ambazo zimekabidhiwa kwenye ofisi ya TAKUKURU ili kifuta jambo hicho wapatiwe wananchi 90 waliopo kwenye kanzidata ambao watapokea kiasi cha Shilingi Milioni moja kila mmoja.

Kizigo ametoa onyo kwa wachimbaji wanaotaka kufanya udanganyifu ili kuongezea majina zaidi ya yale yanayotambulika.

"Wapo wananchi wananipigia simu wakitaja kuwa wao ni sehemu ya kupata kifuta jasho hicho, majina yao hayapo kati ya majina 90 ambayo tumeyapokea kutoka ofisi ya madini, nasisitiza tutafuata kanzidata ya Wizara ya Madini kama Waziri alivyoelekeza," amesema Kizigo.

Waziri Biteko amehitimisha ziara ya siku mbili Mkoani ambapo ametembelea wachimbaji wadogo na kukagua Mgodi wa Kati wa Shanta, kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wadogo pamoja na kutoa elimu ya Sheria ya madini kwa wadau waliojitokeza. Katika ziara hiyo pia aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahembe na Viongozi mbalimbali wa Serikali ya Vijiji na Halmashauri


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...