Sunday, August 1, 2021

Kunambi atimiza ahadi yake ya kujenga Darasa Shule ya Sekondari Londo

AMETEKELEZA! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mbunge wa Jimbo la Mlimba Morogoro, Godwin Kunambi kukabidhi chumba kimoja cha Darasa kwenye Shule ya Sekondari ya Londo iliyopo Kata ya Mbingu jimboni humo.

Ujenzi wa Darasa hilo umetokana na ahadi ya Mbunge Kunambi alipofanya ziara ya kusikiliza changamoto za wananchi wa kata hiyo ambapo alikutana na changamoto katika Shule hiyo ambapo aliahidi kufanikisha ujenzi wake pamoja kuwasilisha changamoto ya uhaba wa walimu.

Katika ajira mpya za walimu zilizotolewa na Serikali, Shule hiyo ya Londo imepata walimu watatu ambao wamepunguza uhaba wa walimu jambo ambalo Mbunge Kunambi aliahidi kulishughulikia pia katika ziara yake ya mwezi Februari.


Akizungumza baada ya kufika katika Shule hiyo, Kunambi amesema baada ya kukamilika kwa Darasa hilo na kupatikana kwa Walimu watatu ni wajibu wake na wananchi kushirikiana katika kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya Walimu ambayo ni changamoto shuleni hapo.

" Ni jambo la faraja kuona tumekamilisha ujenzi wa Darasa hili ambalo limegharimu Sh Milioni 10, niishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kuwezesha pia kutupatia Walimu watatu na hivyo kuondoa changamoto ya uhaba wa walimu iliyokua ikitukabili.

Ni wazi sasa tunapaswa kuhakikisha tunahamishia Nguvu zetu katika kuinua elimu katika Shule yetu ya Londo na Jimbo letu kwa ujumla, tujenge miundombinu bora kwa wanafunzi wetu ambayo itasaidia kukuza ufaulu wao," Amesema Kunambi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo, Nestor Kyelula amempongeza Mbunge Kunambi kwa kufanikisha ujenzi wa Darasa hilo huku akimuahidi kuendelea kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo waliinadi pamoja.

" Kwa kweli umetushika mkono kwa kiwango kikubwa Mhe Mbunge, tulikua na uhaba wa madarasa lakini kupata Darasa hili kwetu ni mchango mkubwa, tukuhakikishie Kupambana kwa pamoja na Walimu wetu katika kuongeza ufaulu wa wanafunzi wetu," Amesema Kyelula.

Nae mmoja wa Wanafunzi wa kidato cha pili shuleni hapo amemshukuru Mbunge huyo kwa mchango wake akisema umeweka alama mioyoni mwao na kuongeza ari ya kusoma kwa bidii ili na wao waje kuwa viongozi watakaosaidia Jimbo la Mlimba.

 

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...