Chama cha Mapinduzi kimesikitishwa na upotoshwaji mkubwa uliyofanywa na gazeti la Uhuru toleo Namba 24084 la leo Jumatano 11 Agosti, 2021, gazeti hili limepotosha sehemu ya mahojiano aliyofanya Rais Samia Suluhu Hassan na BBC.
Katika habari yake kuu limeandika kichwa cha habari "Sina wazo kuwania urais 2025- Samia" Huu ni upotoshwaji mkubwa na kumlisha maneno Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan hakusema kabisa maneno hayo, hili ni kosa kubwa linalokwenda kinyume na sera inayoongoza vyombo hivyo, jambo ambalo halitavumiliwa hata kidogo hivyo HATUA KALI za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya wote waliohusika katika uandaaji wake.
Gazeti la Uhuru ndiyo "Adam na Hawa" wa magazeti yote hapa nchini, linawajibika kuonesha weledi wa hali ya juu na sio vinginevyo.
Tunawaomba Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na watanzania kwa ujumla kupuuza habari hiyo kwani imeandikwa na watu wenye maslahi yao binafsi.
"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan fikra na nguvu zake kwa sasa zimejikita katika kuwatumikia watanzania na si vinginevyo" Shaka Hamdu Shaka