Wednesday, August 11, 2021

Balozi Agnes Kayola aongoza ujumbe wa Tanzania kwenye kikao cha kamati ya kudumu ya Makatibu Wakuu wa SADC

Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu ni miongoni mwa vikao vya awali kuelekea Mkutano wa 41 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika tarehe 17 hadi 18 Agosti 2021 jijini Lilongwe, Malawi.

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu unaongozwa na Mratibu Mkuu wa Kitaifa wa masuala ya SADC, Balozi Agnes Kayola ambaye amemuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine.

Viongozi wengine walioambatana na  Balozi Kayola kwenye mkutano huo ni pamoja na: Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Shaaban ambaye ameongoza Kikao cha Kamati ya Fedha katika kikao hicho cha Makatibu Wakuu; na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa.

Aidha, mkutano huu utafuatiwa na mikutano mingine ya awali ikiwamo Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utafanyika tarehe 13 hadi 14 Agosti, 2021 na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC utakaofanyika tarehe 16 Agosti 2021 ambao utajadili hali ya ulinzi na usalama katika kanda kwa kipindi cha Agosti 2020 hadi Agosti 2021. Mkutano huu utahusisha nchi tatu (3) za SADC Organ Troika ambazo wajumbe wake ni Botswana, Mwenyekiti wa sasa wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama; Afrika Kusini, Mwenyekiti ajaye wa Organ; na Zimbabwe, Mjumbe aliyemaliza muda wa uenyekiti wa Asasi.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa ngazi ya Mawaziri utaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula ambaye ataambatana na Waziri wa Fedha na Mipango, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwakilishi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Mikutano hii ya awali pamoja na mambo mengine inajukumu la kuandaa, kupitia na kuwasilisha mapendekezo ya masuala mbalimbali ya kikanda yatakayofanyiwa maamuzi kwenye Mkutano wa 41 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika utakaofanyika tarehe 17-18 Agosti 2021 jijini Lilongwe.

Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu ulianza tarehe 9 Agosti 2021 na unatarajiwa kumalizika leo tarehe 11 Agosti 2021. Kumalizika kwa mkutano huu kunaruhusu kuanza kwa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

 

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...