Tuesday, May 25, 2021

Tanzania yaweka rekodi mauzo ya dhahabu



TANZANIA imeuza nje dhahabu yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni tatu (takribani shilingi trilioni 7 za Tanzania) kuanzia Aprili mwaka jana hadi Machi mwaka huu.

Kati ya mwaka 2019 hadi 2020 Tanzania iliuza nje dhahabu ya Dola za Marekani bilioni 2.3.

Katibu Mtendaji wa chemba ya migodi Tanzania, Gerald Mturi alisema hayo alipozungumza na HabariLEO.

Mturi alisema, uchambuzi uliofanywa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni kulinganisha kipindi kilichopita cha kuanzia Aprili 2020 na kipindi hiki kilichoishia Machi mwaka huu ikiwa ni sawa na miezi 12.


 
Kwa mujibu wa Mturi kiasi hicho cha mauzo hakijawahi kufikiwa tangu Tanzania ianze kuuza dhahabu nje ya nchi.

Alisema mauzo makubwa ya dhahabu nje ya nchi yalianza baada ya kufunguliwa kwa migodi mikubwa hasa kuanzia mwaka 1999.

Mturi alisema mambo yaliyochangia kuongezeka kwa mauzo hayo ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji kutoka kwa wachimbaji wadogo na janga la ugonjwa wa Covid-19 kuanzia Desemba mwaka 2019 nchini China na madhara yake kuanza kujitokeza nchini Machi mwaka jana.


Mturi alisema kuanzia wakati huo bei ya dhahabu ilianza kupanda kwa sababu katika nchi zilizoendelea ikiwemo Marekani, Uingereza, Japan, Australia na nchi nyingine za Ulaya, wawekezaji wanawekeza fedha kwenye masoko ya hisa.

Alisema katika nchi hizo uwekezaji mkubwa unafanyika kwenye masoko ya hisa kama ilivyo kwenye soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) ambako watu hununua hisa za kampuni.

"Sasa kunapotokea majanga ya kidunia  kama ugonjwa wa corona au vita, thamani ya hisa kwenye masoko hayo huwa zinaporomoka, siku zote huwa hivyo, sasa zinapoporomoka thamani ya hisa zinasababisha wawekezaji kutoa hela zao kule, wanakimbilia kununua dhahabu kwa sababu inaaminika kwamba dhahabu ina uwezo wa kutunza thamani ya fedha,"alisema Mturi na kuongeza;

"Kwa hiyo unanunua dhahabu unakaa nayo miaka miwili au mitatu baadaye unaiuza, sasa kwa kuwa wengi walikuwa wanatoa fedha zao kwenye masoko ya hisa na kuwekeza kwenye kununua dhahabu, ikalazamisha bei ya dhahabu kupanda juu kutokana na uhitaji na mpaka sasa hivi bei bado iko juu."


 
Mturi alisema bei ya dhahabu itaendelea kuwa juu mpaka ugonjwa wa Covid-19 utakapodhibitiwa ndipo uwekezaji mkubwa utarejea kwenye masoko ya hisa na kusababisha bei ya dhahabu kushuka.

Alisema wakati bei ilipoanza kupanda, wakia moja ilikuwa inauzwa kwa Dola za Marekani 1,300 Desemba 2019 na kwa sasa bei ya wakia moja ni Dola za Marekani 1,800 ingawa kuna wakati bei ilipanda hadi kufikia Dola 2,000 za Marekani kwa wakia moja.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...