Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi (TPLB) na Azam Media Limited kwa pamoja wameingia makubaliano ya kuonesha matangazo ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa muda wa miaka 10.
Pande hizo zimesaini makubaliano ya mkataba huo hii leo Mei 24, 2021 jijini Dar es salaam.
Thamani ya mkataba huu ni kwa ajili ya maendeleo ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kwa kutambua hilo, fedha ambayo imewekezwa katika mkataba huu, asilimia 67 itakwenda moja kwa moja kwa timu ambazo zinashiriki ligi hiyo.
Kwa ufafanuzi zaidi ni kuwa kwa msimu ujao yaani 2021/2022, Azam Media Limited itatoa Shilingi bilioni 12, huku timu zinazoshiriki katika Ligi Kuu Tanzania Bara zikipata Shilingi bilioni nane, mgao mwingine utakwenda kwa maendeleo ya soka, TFF na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB).
Fedha hizo zitaendelea kuongezeka kwa kila msimu na msimu wa mwisho wa mkataba yaani 2030/2031, Azam itatoa Shilingi bilioni 28 na wakati huo timu zote kwa ujumla zitapata takribani Shilingi bilioni 19.
Lakini pia kiwango ambacho kitatolewa msimu ujao kitaongezeka zaidi ya mara mbili mpaka itakapofika msimu wa mwisho wa mkataba. Na kila nafasi ambayo timu imemaliza katika Ligi Kuu Tanzania Bara itakuwa na bonasi ambayo itatolewa kulingana na nafasi ya timu kwenye msimamo wa ligi.
Kwa misimu mitatu ijayo yaani 2021/22 mpaka 2023/24, bingwa wa Tanzania Bara atakuwa akipata Shilingi milioni 500 kwa msimu. Mshindi wa pili Shilingi milioni 250, mshindi wa tatu Shilingi milioni 225 na mshindi wa nne Shilingi milioni 200.
Fedha hizo zitakuwa zikiongezeka kila msimu na ndio maana msimu wa 2028/29 mpaka 2030/31 bingwa atakuwa akipata Shilingi milioni 700 kwa msimu. Mshindi wa pili Shilingi milioni 325, mshindi wa tatu Shilingi milioni 275 na mshindi wa nne Shilingi milioni 250.