Tuesday, May 25, 2021

Balozi wa Ufaransa nchini awahimiza Watanzania kujifunza lugha ya Kifaransa

UBALOZI wa Ufaransa nchini Tanzania umezindua maktaba mpya na ya kisasa ambayo itatumika kwa ajili ya kufundishia lugha ya Kifaransa huku ubalozi huo ukitoa mwito kwa Watanzania kujifunza lugha hiyo pendwa ambayo inazungumzwa na mamilioni ya watu duniani kote.

Akizungumza leo Mei 25,2021 baada ya kuzinduliwa kwa maktaba hiyo yenye kila aina ya vifaa vya kufundishia vikiwemo vitabu vya Kifaransa na Kiswahili pamoja na vifaa vya teknolojia ya mawasiliano , Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Fr'deric Clavier amesema maktaba hiyo ipo katika ukumbi wao wa Alliance de France jijini Dar es Salaam.


"Maktaba hii mpya na ya kisasa ambayo iko hapa Alliance de France itatumika kwa ajili ya kufundishia lugha ya Kifaransa, lakini kuwa itawezesha kufanikisha mkakati wetu wa kwamba kwa mwaka tunataka watu 150 wawe wamejifunza Kifaransa kutoka watu 100 kwa sasa.Ni maktaba ambayo ina kila kitu kuanzia vitabu pamoja na aina nyingine za vifaa vya kieletroniki ambavyo vitasaidia katika ufundishaji.


"Nitumie fursa hii kutoa rai kwa wanafunzi kutoka shule na vyuo mbalimbali kuitumia vema maktaba hii kujisomea na kujifunza lugha ya Kifaransa lakini pia hata lugha ya Kiswahili ambayo nayo iko kwenye orodha ya lugha ambazo zinazungumzwa na kupendwa, hata Ufaransa kuna vyuo vingi vinafundisha Kiswahili,"amesema Balozi Clavier.


Katika uzinduzi huo wa maktaba ulikwenda sambamba na utoaji vyeti kwa wahitimu wa lugha ya Kifaransa ambao wamehitimu kwa hatua mbalimbali ambapo amesisitiza lengo la ubalozi huo ni kuendeleza lugha ya Kifaransa nchini Tanzania lakini kukitangaza na Kiswahili nchini Ufaransa.

Hivyo amesema maktaba hiyo ni uthibitisho kuwa Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi ambapo wananchi wake watazungumza Kifaransa."Kwa hapa Tanzania tunahamasisha na kuitangaza lugha ya Kifaransa na kuwahimiza watu kujifunza, kwa kule Ufaransa tunahimiza wananchi wetu kujifunza lugha ya Kiswahili."

Balozi Clavier amesema ubalozi huo na nchi yake kwa ujumla inatamani kuona siku moja Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi zinazozungumza Kifaransa na kwa mikakati waliyonayo hilo litafanikiwa.


Akizungumzia maktaba hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Alliance de France Dar es Salaaam Anissa Boukerche amesema maktaba hiyo inafungua milango kwa mtanzania kuitumia wakati wowote.

Amefafanua ndani ya maktaba hiyo kuna maeneo ya watu wazima, watoto na wanafunzi ambapo wanaweza kujifunza lugha hiyo au kujisomea kwa utulivu mkubwa."Ubalozi wetu mbali ya kuwa na maktaba hii umekuwa ukitoa ufadhili na mwakani kuna wanafunzi watakwenda kusoma lugha ya Kifaransa nchini Ufaransa.


Wakati huo huo baadhi ya Watanzania ambao wamejifunza lugha hiyo ya Kifaransa na kutunukiwa vyeti ka ngazi mbalimbali za kufahamu lugha hiyo, wamesema umefika wakati kwa Watanzania kuhakikisha wanajua kuzungumza lugha zaidi ya moja kwani dunia ya sasa inamuingiliano mkubwa wa watu kutoka mataifa mbalimbali, hivyo itasaidia kufanya mawasiliano.

Stamilu Chaligha ambaye ametunukiwa cheti baada ya kumaliza kujifunza lugha ya Kifaransa amesema yeye ni msanii wa uigizaji, hivyo anaamini lugha hiyo itamuwezesha kupanua wigo wa kazi zake za sanaa ya uigizaji.Aidha amesema kupitia Kifaransa amejikuta anafahamu lugha nyingi na hasa ambazo zinamuingiliano mkubwa na Kifaransa.

 

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...