Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul, amesema ipo haja kwa vyombo vya habari nchi kuendelea kutangaza fursa za kiuchumi na miradi ya kimkakati inayoendelea kutelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita ili wananchi waifahamu na kutumia fursa zilizopo katika miradi hiyo kujiletea maendeleo.
Mhe. Gekul amesema hayo alipotembelea Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) mwishoni mwa wiki Jijini Dares Salaam na kueleza kuwa Serikali inafanya kazi kubwa ya kutekeleza miradi ya maendeleo hivyo vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuujulisha umma kuhusu utekelezaji huo ili waweze kutumia fursa zilizopo.
Serikali yetu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inafanya kazi kubwa ya kuendeleza miradi mbalimbali ya kimkakati, vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuwajulisha watanzania kuhusu maendeleo ya miradi hiyo, fanyeni hivyo ameleza Naibu Waziri.
Amesema Wizara inaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa vyombo hivyo na kwamba kwa kutangaza mambo mazuri ya nchi kuna faida kubwa kwa sababu wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wataziona fursa zilizopo na kuja kuwekeza nchini jambo litakalofungua fursa zingine za kiuchumi zikiwemo ajira kwa watanzania.
Vyombo vya Habari ni muhimu kutangaza shughuli hizi kwani wawekezaji wanaona jinsi ambavyo Serikali yetu inavyojitahidi kuboresha miundombinu, hii inasaidia kwa kiasi kikubwa kurahisisha uwekezaji, na kwa kufanya hivyo tunawavuta wengi waje wawekeze hapa Tanzania amesema Gekul
Aidha amevitaka vyombo hivyo kufuata sheria na kanuni zilizowekwa ili viweze kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa na kwamba Wizara hiyo itahakikisha inavisimamia vyema katika kazi zao na akisisitiza kuwa endapo kuna changamoto inavikabiri vyombo hivyo basi visisite kuwasiliana na Wizara.