Zabibu ni matunda ambayo huwa na rangi nyekundu , nyeusi na baadhi huweza kuwa na rangi ya kijani , njano na hata pinki pia, lakini kwa hapa Tanzania tumezoea yale ya rangi nyeusi.
Zabibu ni miongoni mwa matunda yenye faida kwa afya ya mwanadamu ikiwa ni pamoja na kuimarisha afya ya mishipa ya damu, hivyo kupunguza nafasi ya kuibuka kwa hatari ya magonjwa ya moyo pamoja na saratani.
Zabibu pia inasifika kwa uwezo wake wa kuongeza damu mwilini pale zinapotumiwa mara kwa mara.
Ulaji wa zabibu pia husaidia kumaliza tatizo la ukosefu wa haja kubwa, kwani ndani yake kuna asili ya nyuzinyuzi ambazo ni muhimu katika umeng'enyaji chakula na kumsaidia mhusika kupata choo kwa urahisi zaidi.
Aidha, matunda haya husaidia katika tiba na kinga ya magonjwa ya ini kutokana na uwezo wake wa kuliongezea ini uwezo wa kuondosha sumu mwilini na kuzalisha nyongo kwa wingi.
Mbali na faida hizo, pia zabibu kutokana na kuwa na sukari ya asili huweza kumsaidia mtu katika kupunguza uchovu wa mwili na kutibu maumivu yasiyokuwa na sababu za moja kwa moja.

