Mbunge wa viti maalum, Halima Mdee amewataka Watanzania kumpa nafasi Rais Samia Suluhu na kuachana na tabia ya kuhoji wanawake wanapokuwa viongozi.
Mdee alitoa kauli hiyo jana Ijumaa Machi 26, 2021 akiwa wilayani Chato Mkoa wa Geita katika shughuli ya kumuaga Hayati John Magufuli.
"Tumepata Rais mpya Samia Suluhu tunaamini atafanya kazi nzuri, watu wampe nafasi kwa sababu tuna tabia ambayo si nzuri sana ya kuhoji wanawake wanapopata nafasi wakati wao ndio wanaofanya kazi kubwa majumbani kuhakikisha wengi wanafika mbali, basi tuamini kwamba rais wetu anaweza kutuletea maendeleo katika nchi yetu."
"Ushauri ambao ninaweza kumpa Rais Samia aangalie mapungufu ya aliyemtangulia hasa masuala ya demokrasia na uhuru wa kujieleza na kuhakikisha anarudisha demokrasia iliyokuwepo kabla ya mwaka 2015 pamoja na changamoto zake," amesema Mdee.
Mdee ambaye alifukuzwa uanachama Chadema pamoja na wenzake 18 wakidaiwa kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum bila ridhaa ya chama hicho amesema, "ninaamini akiwa makamu wa rais kuna vitu alikuwa anaona kwa jicho jingine ambalo rais alikuwa halioni."
"Alikuwa amezungukwa na wapambe na sasa atatumia nafasi hii kuyafanyia kazi mazuri ambayo mtangulizi wake aliyafanya ayaboreshe zaidi."
Source