Watu 25 wameripotiwa kufariki wakiwemo wafungwa 6 kufuatia ghasia zilizotokea wakati wafungwa walipokuwa wakijaribu kutoroka gerezani nchini Haiti.
Kulingana na taarifa za vyombo vya habari, wafungwa ambao walianzisha ghasia katika Gereza la Croix-des-Bouquets karibu na mji mkuu wa Port-au-Prince na kujaribu kutoroka, walipambana na polisi.
Wakati wa makabiliano na vikosi vya usalama, watu 25, wakiwemo wafungwa 6 kati walipoteza maisha, na zaidi ya wafungwa 200 wakatoroka gerezani.
Mamlaka ilitangaza kuwa wafungwa walishambulia raia wakati wa kutoroka gerezani, na kusababisha raia kadhaa kufariki.
Imebainika kuwa polisi wamewakamata wafungwa 69 hadi sasa katika operesheni iliyoanzishwa dhidi ya wafungwa waliotoroka gerezani.
Kwa upande mwingine, inasemekana kwamba mmoja wa viongozi wa magenge yenye silaha huko Haiti alikuwa miongoni mwa wafungwa waliotoroka gerezani.
Rais Jovenel Moise alitoa taarifa kwenye akaunti yake ya Twitter kuhusu tukio hilo na kusema,
"Tunalaani wale waliokimbia kutoka gereza la Croix-des-Bouquets na tunawasihi watu wawe na utulivu. Nimetoa maagizo yote muhimu kwa Polisi wa Kitaifa kudhibiti hali hiyo."
Gereza la Croix-des-Bouquets linatajwa kama mahali pa mfano kwa wapinzani wanaotuhumiwa kujaribu kutekeleza mapinduzi dhidi ya Rais Moise mnamo 7 Februari.