![]()  | 
| MKURUGENZI wa Agri Thamani ambaye Pia ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia NGOs Mh Neema Lugangira akigawa taulo za kike kwa wanafunzi wa shule za Sekondari | 
![]()  | 
| WANAFUNZI wa kike wa shule za Sekondari wakifurahia kupokea mfuko wao uliojaa taulo za kike za kutosha mwaka mzima kwa kila mmoja | 
![]()  | 
| FUSO lililokuwa limejaa Taulo za kike za wanafunzi wa kike 1800 wa Bukoba Manispaa likiingia kwenye uwanja wa Kaitaba Bukoba mjini likitokea Dar es Salaam | 
![]()  | 
| Mabox ya Taulo za kike ambazo zote zilikuwa zimeandikwa Jina la Shule ya Sekondari kwa Idadi Kamili ya Wanafunzi wa Kike | 
Mkurugenzi wa Agri Thamani; Mhe Neema Lugangiea (Mb.)  ambae pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) kupitia Kundi la Asasi za  Kiraia (NGOs) Mh.Neema Lugangira ametoa msaada wa taulo za kike kwa  wanafunzi 1800 kutoka kwenye shule 16 za Manispaa ya Bukoba .
Ambapo  kila mwanafunzi mmoja ataweza kutumia taulo alizopewa kwa kipindi cha  mwaka mmoja katika zoezi ambalo iliyofanyika kwenye uwanja wa Kaitaba  mjini Bukoba.
Kwa  Manispaa ya Bukoba jumla ya packet 25,200 za Taulo za Kike ziligawiwa  kwa Wanafunzi wa Kike 1,800 kutoka Sekondari 16 za Kata zote 14 za  Manispaa ya Bukoba.
Akizungumza  wakati wa ugawaji wa taulo hizo katika zoezi ambalo liliratibiwa na  Idara ya Elimu Sekondari Bukoba Manispaa na Afisa Elimu Taaluma  Sekondari alishiriki zoezi zima.
Mhe  Neema Lugangira amesema ameamua kufanya hivyo ili kuwasaidia wanafunzi  hao kuweza kujihifadhi na kuweza kuendelea na masomo yao wakati wa   kipindi cha hedhi.
Alisema  wanafunzi ambao watanufaika na msaada huo ni kuanzia kidato cha kwanza  hadi cha nne ambao kwa sasa wataondoka na adha ambayo walikuwa  wakikumbana nao wakati wakiwe kwenye kipundi cha hedhi.
"Naamini  msaada huo utakuwa na manufaa makubwa kwao kutokana na kwamba watatumia  muda mwingi kusoma hata wakiwa kwenye kipindi chao cha hedhi kutokana  na kuwa na taulo ambazo zitawasaidia" Alisema Mbunge huyo.
Akizungumzia  kuhusu msaada huo wa Taulo za Kike, Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya  Bukoba Mjini Emanuele Ebeneza alimshukuru Mbunge Neema kwa msaada wake  wa taulo za wasichana ambao utakuwa chachu ya kupunguza utoro shuleni.
Alisema  kupitia msaada huo wanafunzi wengi watajua namna ya kujihifadhi na  kupunguza utoro shuleni kwa sababu ya kutokujisikia vizuri kwenye  kipindi cha hedhi.
"Niseme  tu kwamba licha ya kutoa msaada huo lakini pia Mbunge Neema anafundisha  wanafunzi juu ya hedhi salama,  anawaandaa kisaikolojia kupita kwenye  kipindi cha hedhi na hivyo kuwaondolea hofu na anawapa elimu ya lishe  bora inayowasaidia waepukane na changamoto ya upungufu wa damu (anemia)  "Alisema Afisa Elimu Sekondari Bukoba Manispaa. 
Afisa  Elimu Sekondari huyo alisema kwamba pia Mbunge Neema Lugangira  anawafundisha usafi hatua ambayo inasaidia kupunguza utoro ambao  ungetokana na wanafunzi kushindwa kuhudhuria masomo wakati wa mzunguko  wa hedhi.
"Kama  unavyojua mzunguko wa wasichana unatokea kila mwezi mara moja na wakati  mwengine wakishindwa kuhudhuria masomo hivyo alilolifanya ni kitu cha  muhimu sana sana kwa maana ya wanasichana "Alisema Ndg Ebeneza
Mmoja  wa wanafunzi hao Alisema kwamba changamoto kubwa ni kubwa pale pedi  zinapokuwa zimekwisha wanashindwa kuishi kwa amani kabisa wakati wakiwa  wanaendelea na masomo
Naye  mwanafunzi mwengine amesema wanashukuru kwa msaada huo kutokana na  kwamba wakati mwengine wamekuwa wakikosa shule kutokana na kutokuwa na  taulo za kujihifadhi wakati wakiwa kwenye kipindi cha hedhi.
Hata  hivyo Avitha Faustini ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika  Shule ya Sekondari  Hamugumbe alimshukuru Mbunge Neema kwa msaada huo  ambao amewapatia ambao umekuwa ni faraja kubwa kwao na kuwaondolea  changamoto walizokuwa wakikumbana nazo.
Alisema  wamepata ujasiri wa kuendele na masomo kwani kabla ya kupata Taulo   hizo walikuwa wakitokewa na hali hiyo wanakuwa wanyonge na wakati  mwengine hulazimika kurudi nyumbani na  kukosa masomo. Aliongezea kwamba  sasa hivi hawana haja ya kuwaomba wazazi pesa ya kununua pedi.
Mwanafunzi  mwingine alikiri kwamba wengi hawajawahi kuziona taulo za kike na  alielezea njia ambazo wengi wao wanatumia ambazo kwakweli hata sisi  tunashindwa kuziandika maana sio salama kabisa. Mwanafunzi huyu  alionyesha furaha ya aina yake kuona kwamba wamekumbukwa na kuthaminiwa  hata kama wao ni watoto wa kimaskini.
Mradi  huo wa Taulo za Kike umeshawanufaisha  Watoto wa Kike katika mikoa ya  Dodoma, Tabora, Pwani, Tanga, Kigoma, Mtwara na Kagera na mikoa  inayofuata kwa awamu hii ya kwanza ni Ruvuma na Lindi
Mbunge  Neema Lugangira alimalizia kwa kusema kwamba Jumla ya Wanafunzi wa Kike  5,500 nchini watakuwa wamenufika ifikapo mwezi Mei 2021 ambapo Taulo za  Kike zote zimetengenezwa na Kiwanda cha Tanzania ambacho kinauzoefu wa  zaidi ya miaka 40 kwenye eneo hili. 




