Friday, February 26, 2021

Kocha Simba Aigeukia Yanga, Ligi Kuu na Kombe la FA





KOCHA Mkuu wa Simba, Mfaransa Didier Gomes ameweka kando maandalizi ya mchezo unaofuatia wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al-Merrikh ya nchini Sudan na badala yake nguvu amezirudisha katika Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.

 

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu awafunge mabingwa wa Afrika Al Ahly ya nchini Misri bao 1-0 mchezo uliopigwa Jumanne kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.



Simba hivi sasa ipo katika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi wakiwa na pointi 42 wakiongozwa na Yanga wenye 49 ambao wamepanga kubeba mataji yote wanayoshindania ligi na FA kwenye msimu huu.

 

Kwa maana hiyo ni wazi sasa Gomes akili yake kwa kipindi hiki anawaza ushindi katika ligi za ndani ikiwemo Ligi Kuu ili kuifukuzia Yanga ambao ndio wanapambana nao katika mbio za ubingwa msimu huu.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Gomes alisema kuwa wamepanga kuanza maandalizi ya mchezo dhidi ya Merrikh wiki mbili zijazo na hivi sasa nguvu na akili zake amezielekeza katika ligi kuu na FA.



Gomes alisema ndani ya wakati mmoja anataka kuona anaipa mataji timu hiyo na kubwa ligi, hivyo hivi sasa yupo katika maandalizi ya kukiimarisha kikosi chake kuhakikisha wanaondoa Yanga kileleni kwa kushinda michezo yote iliyokuwepo mbele yao.

 

Aliongeza kuwa anaamini atafanikiwa katika hilo kutokana na ubora wa kikosi chake ambao wameuonyesha katika mchezo wa kimataifa waliocheza dhidi ya Al Ahly uliomalizika kwa Simba kushinda bao 1-0.



"Tumeshinda mechi mbili na tunaongoza Kundi A, ni matokeo muhimu sana kwetu.

Tunaanza maandalizi ya mchezo unaofuata wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al-Merrikh wiki mbili zijazo."Mchezo wetu wa Merreikh hautakuwa mwepesi hii ni timu ninayoifahamu vizuri kutokana na kuwahi kuifundisha, hivyo sina hofu nayo na zaidi hivi sasa nguvu na akili nazihamishia katika ligi na FA.

 

"Hatutakuwa na utani katika michezo inayofuatia ya ligi na kikubwa tunataka kukaa kileleni kwenye msimamo wa ligi na mwisho wa siku tuwe mabingwa, hilo sina hofu nalo kutokana na ubora wa vijana wangu," alisema Gomes.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...