Friday, February 26, 2021

Jafo aeleza chanzo shule za bweni kuteketea kwa moto

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Selemani Jafo amesema chanzo cha mabweni kuteketea kwa moto ni ubovu na uchakavu wa miundombinu.


Ameeleza hayo leo Ijumaa Februari 26, 2021 jijini Dodoma wakati akizindua ushirikiano wa programu ya mafunzo kati ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na chama cha skauti Tanzania.


Amesema maeneo mengi kunaporipotiwa majanga ya moto imekuwa ni ubovu wa miundombinu licha ya kuwa zipo sababu nyingine.


Amebainisha kuwa ili  kudhibiti tatizo hilo, Serikali imeamua kufanya ukarabati wa shule kongwe zote nchini, kwamba zilizoanishwa ni 89 lakini hadi sasa wamefikia 86.


"Kuna uzembe ndani yake, hujuma na mambo mengine lakini kikubwa ni uchakavu wa miundombinu unaotokana na ukongwe wa majengo yetu, lazima tubadilike na kutoka huko sasa maana si wakati wa kurudi nyuma," amesema Jafo.


Jafo ameziagiza shule binafsi kupitia mifuko ya majengo yao upya ili waweze kuchukua tahadhari kabla ya majanga kuwakuta kwani moto umekuwa ukisababisha madhara makubwa kwa shule za Serikali na binafsi.


Amewaagiza wakuu wa shule kutoa ushirikiano kwa mamlaka za uchunguzi ili waliosababisha majanga ya moto wachukuliwe hatua.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...