Hospitali ya Rufaa ya KCMC inayomilikiwa na Shirika la Msamaria Mwema (GSF) imefuta sherehe za maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake zilizokuwa zifanyike Machi mosi hadi 6, 2021.
Sherehe hizo zilikuwa ziambatane na utoaji wa huduma 15 bure kwa wahitaji 5,000 kutoka maeneo mbalimbali Tanzania ikiwa ni pamoja na upimaji wa magonjwa na ushauri bure kwa watakaobainika kuwa na matatizo.
Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Februari 26, 2021 na ofisa uhusiano wa KCMC, Gabriel Chisseo inasema huduma hizo 15 za matibabu zilizokuwa zitolewe bure nazo zimefutwa kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wa KCMC.
"Huduma za matibabu bure na huduma za maonyesho zilizokuwa zimepangwa kutolewa na idara mbalimbali na mashirika alikwa hazitaweza kufanyika kama ilivyokuwa imepangwa kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu," inasema.
Ofisa huyo amesema huduma za kawaida za kitabibu pamoja na kliniki zitaendelea kutolewa kama ilivyo utaratibu wa hospitali na Chisseo kupitia taarifa hiyo amesema uongozi unaomba radhi umma kwa usumbufu utakaojitokeza.
Huduma ambazo KCMC ilikuwa imepanga kuzitoa bure kama sehemu ya maadhimisho hayo ni upimaji mkojo kwa utambuzi wa shida ya figo na pia wangepima maambukizi ya virusi ya Ukimwi na saratani ya shingo ya kizazi.
"KCMC ilikuwa imepanga kupima bure saratani ya matiti na kutoa elimu ya afya ya mama na mtoto na kutoa elimu pia ya magonjwa ya upasuaji, tezi dume, elimu ya magonjwa ya njia ya mkojo, chakula na lishe na elimu ya uzazi," inaeleza taarifa hiyo.
Hospitali hiyo ilikuwa itumie maadhimisho hayo pia kufanya harambee ya uchangiaji wa taasisi ya moyo kanda ya Kaskazini inayojengwa KCMC kwa gharama ya Sh16 bilioni ambayo ni muhimu kwa kanda ya Kaskazini.
KCMC anayotegemewa na watu zaidi ya milioni 15 wa mikoa ya Kaskazini ilianzishwa mwaka 1971 ikiwa na vitanda 300 tu vya kulaza wagonjwa, lakini sasa ina vitanda 686 ikipokea wagonjwa wa nje 1,000 kila siku.