Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko (juu pichani)
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Shinyanga kuwaomba Radhi wananchi kutokana na kukata umeme mara kwa mara bila kutoa taarifa ili wafahamu kinachoendelea.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa agizo hilo leo Ijumaa Februari 26,2021 baada ya kukerwa kitendo cha TANESCO kukata umeme bila kutoa taarifa kwa wananchi kwani inaathiri biashara na shughuli za kijamii.
"Namuagiza Meneja wa TANESCO mkoa wa Shinyanga awaombe radhi wananchi kwa kutotoa taarifa kuhusu kukatika kwa umeme na aeleze kwanini umeme unakuwa hivi, kwanini umeme unakatika mara kwa mara Shinyanga",amesema Mboneko.
Mboneko ameyataja maeneo yanayolalamikiwa zaidi kwa kukatiwa umeme katika Manispaa ya Shinyanga kuwa ni Kitangiri, Ndala, Ibinzamata, Mwawaza na Masekelo pamoja na maeneo mengine Mjini Shinyanga ambapo umeme umekuwa ukikatwa.
Aidha amemtaka Meneja huyo wa TANESCO kusimamia kikamilifu Idara ya Uhusiano na Huduma kwa Wateja ya TANESCO iwe inatoa taarifa kwa wananchi kuhusu kukatika kwa umeme kupitia vyombo vya habari zikiwemo Redio za Kijamii na Mitandao ya kijamii ili wananchi wafahamu nini kinaendelea badala ya kukaa tu kimya.
"Meneja wa TANESCO akae na maafisa habari wa TANESCO wawe wanatoa taarifa kuhusu kukatika kwa umeme kwenye vyombo vya habari zikiwemo Redio za Kijamii kama vile Radio Faraja,mitandao ya kijamii yakiwemo magroup ya Whatsapp ama watume Ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kwa wananchi ili wajue kinachoendelea kama inavyofanya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Shinyanga (SHUWASA)",amesema Mboneko.
"Tofauti na changamoto ya Gridi ya Taifa ambapo umeme hukatika nchi nzima, hapa Shinyanga tupewe taarifa za kukatika kwa umeme. Haiwezekani maeneo mengine yawe na umeme halafu Shinyanga umeme unakatika na hakuna taarifa yoyote inatolewa",ameeleza Mboneko.
Katika hatua nyingine, Mboneko ameiagiza TANESCO mkoa wa Shinyanga kuboresha Kitengo cha Huduma za Dharura (Emergency) kwani kuna malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa wanapopigiwa simu kuhusu matatizo ya umeme hawafiki kwa wakati na inafikia wakati wanaenda baada ya hata siku tatu hadi wiki moja.
Pia amewataka kuondoa nguzo zilizokuwa zinatumika kupitishia umeme kuziondoa kwenye baadhi ya maeneo baada ya kuweka nguzo mpya baada ya kufanya maboresho na kuhakikisha maeneo yasiyo na huduma ya umeme yanapelekewa umeme.
"Kata za Mwamalili na Masengwa ziingizwe kwenye miradi ya REA lakini maeneo mengine ambayo hayana umeme katika Manispaa ya Shinyanga TANESCO wafanye survey na makisio wapeleke Wizarani, sisi tufuatilie kuomba hizo fedha",amesema Mboneko.
Hali kadhalika ametaka TANESCO ifuatilie na kuwajua wananchi waliolipia huduma ya umeme na hawajafungiwa umeme mpaka leo kama vile Kolandoto na viwanja vya Mwadui kata ya Ngokolo na kuhakikisha wanatoa Control Number kwa wakati.
Nao wananchi wamesema wanakerwa na kitendo cha kukatwa umeme mara kwa mara hususani inapofika saa moja usiku umeme unakatwa kusababisha vifaa vya umeme kuungua,hivyo kuiomba TANESCO kuwa inatoa taarifa kwa wananchi.
"Ni matengenezo gani wanafanya kila siku wanakata umeme?.. wakati mwingine wakata umeme kisha wanarudisha ndani ya sekunde 30. Kama ni mgao wa umeme ni mgao gani huu, huu mtindo wa kukata umeme kwa sekunde nao unaitwaje",wamehoji wananchi.
Hata hivyo Mwandishi wa habari hizi alipomtafuta Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Narrowil Sabaya kuzungumzia malalamiko ya wananchi kuhusu ukataji umeme na chanzo cha umeme kukatika mara kwa mara amesema atatoa taarifa.