Na Ezekiel Mtonyole - Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge ametoa zawadi ya sikukuu ya Christmas kwa makundi maalumu ya watoto wenye mahitaji maalumu na watoto yatima katika mkoa wa Dodoma ikiwa ni katika kusherekea siku hiyo.
Miongoni mwa vituo vilivyonufaika na zawadi hizo ni kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu wa viungo cha Mlali Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma, kituo cha kulelea watoto yatima cha Rahman kilichopo Chang'ombe Jijini Dodoma.
Akikabidhi zawadi hizo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, afisa mawasiliano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa bwana Jeremiah Mwakyoma amesema Mkuu ameamua kutoa zawadi hizo ili watoto nao wa sherekee Sikukuu hiyo vizuri na kutumia nafasi hiyo kuwatakia sikukuu njema wananchi wote na kuwataka kusherekea kwa utulivu na amani.
"Mkuu wetu wa mkoa ni kawaida yake kutoa zawadi kama hizi kwa makundi kama haya lengo lake ni kuona makundi haya nayo yanajiona ni sehemu ya jamii" amesema.
Amewataka watu binafsi mashirika na taasisi mbalimbali kuwa na moyo wa kuyakumbuka makundi hayo kwani ni watu wanaohitaji faraja na kujiona nao wanathaminika katika Jamii.
Amebainisha kuwa serikali yake ya mkoa itaendelea kuwaunga mkono watu binafsi, taasisi na mashirika yanayojihusisha na kuyasaidia makundi hayo kwa kuyasaidia kutoa elimu na vituo vinavyosaidia kuwalea watoto hao.
Baadhi ya wanaohudumia makundi hayo kikiwamo kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu kilichopo Mlali Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma Mkurugenzi wa kituo Padri Gaudence Shayo amemshukuru Mkuu wa Mkoa huyo kwa moyo alionao wa kuyakumbuka makundi hayo hasa katika kipindi hiki cha Sikukuu.
"Sio wote wenye moyo kama huu Mungu amzindishie kwa siku kama hii watoto watafurahi kwa zawadi hii ambayo Mkuu wa Mkoa ameamua kusherekea nao" amesema Padri Shayo.
Nae mlezi wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Rahman kilichopo Chang'ombe Jijini Dodoma, Rukia Khamis amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuwa na moyo ya kukumbuka hata vituo dini tofauti katika kusherekea sikukuu hiyo kuwa huo ni mfano wa kuigwa na wengine.