Saturday, December 26, 2020

Amber Rutty; Kinachokosekana Siyo Milioni 3 Za Kumtoa Jela Ila…




MAKOSA matatu aliyokutwa nayo msanii Rutyfiya Abubakary almaarufu Amber Rutty likiwemo la kufanya mapenzi kinyume na maumbile, yametosha kumfanya awe mfungwa wa miaka mitano gerezani.

 

Kwa huruma na jicho la upendo na uzito wa kosa lenyewe, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Godfrey Isaya alisema siku anatoa hukumu yake;

 

"Nimezingatia hoja za pande zote mbili na athari za makosa haya, ni kweli washitakiwa wote ni vijana na wanategemewa, nimeona mshitakiwa wa kwanza anajutia, mshitakiwa wa pili na tatu ni wakosaji wa kwanza, kutokana na mazingira ya kesi hii adhabu yake ni miaka 30 kila kosa ambapo nikiwafunga mtapotea kabisa.

 

"Hivyo kwa mazingira mliyoyasema na lengo la adhabu ni kujirudi, mshitakiwa wa kwanza utalipa shilingi milioni 3 au jela miaka 5, wa pili utalipa faini ya shilingi milioni 3 au jela miaka 5 na mshitakiwa wa tatu faini shilingi milioni 5 au jela miaka 5."

 

Hii ndiyo ilikuwa hukumu ya Amber Rutty, mpenzi wake, Said Bakary pamoja na James Charles (James Delicious). James alilipa faini na kumwacha Amber Rutty na mpenzi wake wakiendelea na msoto kwenye Gereza la Segerea jijini Dar.

 

Mara nyingi nimekutana na baadhi ya wasanii na kuwasikia jinsi ambavyo wanaumizwa na msanii mwenzao, Amber Rutty kusota gerezani, lakini ukiwaangalia kuna jambo la ziada unajifunza.

 

Maana kinachomfanya msanii huyo kuendelea kutaabika gerezani ni shilingi milioni tatu na kwamba zikitolewa hata kesho anakuwa uraiani.

 

Lakini cha kusikitisha ni kwamba wasanii wote kwa umoja wao mpaka sasa wamemkunjia mikono na ni kama wanasema; "Kufa na lako!"

 

Hawana pesa za kumsadia? Jibu ni kwamba wanazo kwani baadhi wanaonekana mitaani wakila bata kanakwamba hakuna kilichomkuta mwenzao.

 

Nini kilicho nyuma ya ukimya wa wasanii wenzake kumpa kisogo mwenzao kiasi cha kumwacha aangamie gerezani? "Ni hukumu ya kibinadamu."

 

Hakimu Isaya alipokuwa akiwahukumu aliwatazama usoni na kugundua kuwa watuhumiwa walikuwa wanajutia makosa hivyo kwa nafasi yake aliamua kuwahurumia kwa kutowapa kifungo cha miaka 30 ila aliwapiga mitano yenye nafuu ya faini.

 

Hakimu Isaya ni kama aliwaambia wasanii wenzake na Amber Rutty; "Mimi nimeshatoa mchango wangu wa huruma, kazi kwenu kumalizia palipobaki."

 

Lakini hadi sasa si Wema Sepetu, Kajala Masanja, Ray Kigosi, Johari, Steve Nyerere, JB, Wolper na Uwoya waliojitokeza na kuonesha huruma kwa mwanamke huyo ambaye ni maarufu kwa kiasi chake hapa nchini.

 

Hata Diamond, Harmonize, Nandy, Zuchu, Lady Jaydee, nao huruma bado haijawaingia kuweza kumsadia kijana mwenzao atoke ili maisha yaendelee.

 

Nilimuuliza mmoja wa wasanii wakubwa nchini (jina ninalificha) ni kwa nini kwa Lulu aliyekutwa na hatia ya kumuua bila kukusudia muigizaji nguli nchini Steven Kanumba. huruma kwake ilikuwa kubwa miongoni mwa jamii hadi akapiganiwa kila kona atoke gerezani?

 

Msanii huyo alinijibu; "Ni aina ya kosa alilofanya Amber Rutty ndilo linalowagopesha watu kujitokeza hadharani kwenda kumsaidia."

 

Nikajiuliza; "Kosa hilo ni lipi?" Ni hilo la usodoma na ugomora eeeeh?

Msanii huyo alinijibu wewe unadhani ukijitokeza kumsaidia Amber Rutty watu si watasema; "unataka umtoe ili ujilie vyako."

 

Nikajua kuwa kumbe tatizo siyo pesa ni kosa la Amber Rutty ndilo linalomfanya aendelee kusota gerezani na kwamba watu hawataki kufungamanishwa nalo.

 

Siku za hivi karibuni Mchungaji Mashimo alijitokeza na kuanzisha harambee ya kumchagia Amber Rutty atoke gerezani, lakini hakupata hata senti kumi, kwani watu wanaogopa kuambiwa wamemchangia 'msodoma'.

 

Baba mzazi wa Diamond, mzee Abdul alipokwenda kumjulia hali Amber Rutty gerezani hivi karibuni alimwaga chozi, akarudi na harakati za kutaka kumchangishia pesa ili atoke, naye akaambulia patupu.

 

Ujumbe wangu kwa watu wote ni kwamba sisi sote ni wakosaji, tuwe watu wa kusameheana na kutakiana heri bila kuhukumiana.

 

Ni wazi Amber Rutty kama binadamu aliteleza, alikengeuka, lakini sitaki kuamini kuwa anapaswa kutengwa na jamii. Ni wazi anahitaji mtu wa kumshika mkono ili aanze maisha mapya na ikumbukwe bado anao ndugu ambao wanaumizwa na kifungo chake.

 

Hivi karibuni baba yake mzee Abubakary amemlilia mwanaye na kuwaomba Watanzania wamsaidie maana yeye mikono yake ni mitupu na kwamba hawezi kumuokoa mwanaye na janga hilo zito.

 

Kupitia makala haya nitoe wito kwa wasanii na watu wote kujitokeza kumsaidia msanii huyo bila kuogopa binadamu watasemaje kwa sababu mlipa wema ni Mungu na wanadamu tunabaki kuwa wote ni wakosaji.

0714 895 555.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...