Mgombea wa urais nchini Uganda Robert Kyagulanyi, anayefahamika zaidi kama Bobi Wine, ameahirisha kampeni zake, kufuatia kujeruhiwa kwa maafisa wake wa kampeni na kuharibiwa kwa gari lake.
Kiongozi huyo wa upinzani anasema isasi zilifyatuliwa kwenye gari lake na kutoboa matairi ya gari lake na kumfanya asiweze kusafiri tena.
Video zilizosambazwa na timu yake ya kampeni kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha kitu ambacho hakikutambuliwa kikilipuka umbali wa mita kadhaa kutoka mahali alipokuwa.
Awali katika eneo la Kayunga, mashariki mwa Kampala, gesi za kutoa machozi zilitumika kuwatawanya wafuasi wake.
Maafisa wanne wa kampeni yake walijeruhiwa. Mmoja wao, aliyetambuliwa kama producer Dan Magic alipigwa usoni. Mmoja wa polisi wanaowalinda wagombea wa urais waliotolewa na Tume ya Uchaguzi pia alijeruhiwa.
Takriban wiki mbili zilizopita, watu 54 waliuawa wakati wafuasi wa mgombea huyo walipokuwa wakiandamana kudai aachiliwe huru baada ya kukamatwa na polisi katika mkutano wa kampeni.
Baadaye alishitakiwa kwa kukiuka masharti ya kukabiliana na janga la corona kwa kukusanya umati wa watu na baadaye akaachiliwa kwa dhamana.
Vikosi vya usalama vimeendelea kuzuwia mikutano yake ya kisiasa pamoja na ya wanasiasa wengine wa upinzani.
Katika hotuba yake ya kitaifa Jumapili, Rais Yoweri Museveni, aliwatetea polisi na jeshi akisema kuwa hakuna mwanasiasa yoyote ambaye hawezi kuguswa.
Kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa mwezi Januari, zimeendelea kuchacha huku na kuelekezwa zaidi katika jiji kuu la Kampala.