MWANASHERIA mkuu wa Marekani, William Barr, amepigilia msumari wa mwisho kwenye sakata la uchaguzi baada ya kusema kwamba wizara ya sheria haijapata ushahidi wowote wa kufanyika udanganyifu katika hesabu ya kura kwa uchaguzi mkuu wa Marekani uliofanyika 3 Novemba, 2020.
Barr amesema kwamba wizara hiyo haijapata sababu yoyote inayoweza kubadilisha matokeo ya uchaguzi huo.
Ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba waendesha mashtaka wa Marekani wamekuwa wakishirikiana na maafisa wa shirika la upelelezi nchini humo (FBI) kufuatilia madai yaliyokuwa yametolewa kuhusu uchaguzi huo lakini hakuna ushahidi wowote ambao umepatikana.
Haya yanajiri wakati Rais Donald Trump anaendelea kutoa madai kwamba kulifanyika wizi wa kura, na kukataa kukubali kwamba alishindwa na Rais Mteule, Joe Biden.
Barr ni mmoja wa washirika wa karibu sana wa Trump na aliagiza wanasheria wa serikali kote nchini kuchunguza madai ya wizi wa kura iwapo ulifanyika.
Wakati huo huo, Biden ameahidi kuujenga uchumi wa Marekani utakaowanufaisha Wamarekani wote, wakati atakapoingia madarakani Januari 20, 2020.
Uchumi wa Marekani kwasasa unakabiliwa na tisho la janga la virusi vya Corona.
Source