Sunday, November 8, 2020

Polisi Dar wataja sababu kesi za unyanyasaji kutofika mwisho

 


Licha ya kupokea taarifa na malalamiko mengi dhidi ya watoto wanaofanyiwa ukatili, Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam kupitia dawati la jinsia, limesema bado linakutana na changamoto ya kesi hizo kutofika mwisho.


Mkuu wa dawati hilo, Mrakibu mwandamizi wa Polisi, Leah Mbunda, alisema licha ya kupata taarifa za ukatili dhidi ya watoto na kuzishugulikia, wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali, ikiwamo kesi nyingi zinazoripotiwa kutofikia mwisho mzuri, kwa sababu zikishafika mahakamani waathirika hawaonekani.


Mbunda alisema hayo, wakati Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC) kilipotoa elimu juu ya madhara ya ukatili dhidi ya watoto sambamba na kukumbuka siku ya mtoto wa kike iliyofanyika katika shule ya msingi Mbagala.


Mbunda alitaja matukio yanayoongozwa kuripotiwa katika madawati ya jinsia yaliyopo katika Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kuwa ni malalamiko ya malezi ya watoto, kubakwa kwa watoto na kulawitiwa.


Matukio mengine ni malalamiko ya malezi ya watoto na kwamba matukio ya kubakwa na kulawitiwa, yamekuwa yakitokea zaidi katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu pamoja na maeneo ya makazi ya watu wenye kipato cha chini.


"Kwa sasa wananchi wamehamasika zaidi katika kuripoti matukio ya ukatili katika madawati ya jinsia, tofauti na ilivyokuwa katika miaka ya nyuma na hii inatokana na wananachi kuwa na uelewa, ndio maana wanajitokeza kwa wingi katika vituo vya polisi kutoa taarifa" alisema Mbunda.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...