SIKIA hii hapa; tambiko limemuibulia zengwe aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joshua Nassari, uhondo wa stori unakuja.
Nassari ambaye hivi karibuni alikihama Chadema na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), alichukua fomu za kuomba uteuzi wa ubunge ndani ya CCM kwenye jimbo lake la zamani ambapo aliipeleka kwa Wazee wa Mila maarufu kama Washili ili ikatambikiwe.
Mbali na fomu hiyo kupelekwa huko, Nassari aliichukua pia hadi kanisani na kuwakabidhi wachungaji nao waiombee apate kushinda kwenye kura za maoni CCM ili baadaye awanie ubunge kupitia chama hicho.
Mara paap, Nassari aliangukia pua kwenye kura hizo za maoni kwa kupata kura 26 na mshindi kuibuka Dk. John Pallangyo.Baada ya matokeo hayo, zengwe la tambiko lilipata nguvu kwenye mitandao ya kijamii ambapo wengi walimponda mwanasiasa huyo kijana kwa kujihusisha na imani za kale.
"Kijana unaamini tambiko kwenye kitu makini kama uchaguzi, huku ni kufilisika kimawazo," aliandika mtu mmoja kwenye ukurasa wake wa Instagram.Hata hivyo, jicho la Amani Mtandaoni limebaini kuwa, Nassari ni miongoni mwa wagombea ubunge ndani ya CCM aliyesemwa vibaya baada ya kushindwa kura za maoni.
Uchunguzi umebaini kuwa, hayo yanatokana na mitazamo kinzani baina ya wafuasi wa Chadema ambao wanamuona Nassari kama msaliti wa chama na CCM ambao wanampa tano kwa uamuzi wake.
Ingawa tambiko na masuala ya mila hayakatazwi kisheria, wengi walimshambulia Nassari kwa kitendo chake hicho wakifananisha jambo hilo na masuala ya ushirikina, kitu ambacho sivyo kilivyo.Julai 17, mwaka huu, mbunge huyo wa zamani alichukua fomu katika ofisi za CCM Usa River, halmashauri ya Meru na kuipeleka moja kwa moja kwa wazee wa ukoo.
Akiwa ameambatana na wapambe wake, Nassari aliikabidhi fomu hiyo kwa wazee hao wa kimila ambao waliitambikia chini ya mti mkubwa ambao hutumiwa kwa shughuli za mila.Aidha, baada ya shughuli ya kimila kumalizika, Nassari aliongozana na wapambe wake hadi kanisani ambako aliangushiwa maombi ili ashinde uchaguzi, jambo ambalo halikuwezekana