Wednesday, April 1, 2020

Vitakasa mikono vyaanza kuzalishwa Manyara

Katika kuimarisha mapambano na kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti ameagiza uongozi wa kampuni ya Matisuperbrand ya mjini Babati inayozalisha pombe kali kusambaza mara moja vitakasa mikono katika maeneo yenye changamoto ya maji baada ya kampuni hiyo kuanza uzalishaji wa bidhaa hiyo.

Mnyeti akiwa na kamati ya usalama ya mkoa wa Manyara amesema kuwa wananchi waliopo maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa maji ndiyo waliopo hatarini zaidi kuambukizwa virusi vya Corona huku pia akionyesha kusikitishwa na baadhi ya taasisi za serikali kuchukua muda mrefu katika kuruhusu viwanda kuanza kusambaza bidhaa hiyo muhimu kwa kipindi hiki cha janga la Corona baada ya kampuni hii kumueleza kuchelewa kupatiwa ridhaa ya kuanza kusambaza licha vitakasa mikono hivi kuthibitishwa ubora.

Nao wajumbe wa kamati hii ya usalama wakaeleza kufurahishwa na hatua ya kiwanda hiki kuzalisha sanitizer hususan katika kipindi hiki.

Jeshi la polisi nalo mkoani hapa likaonya watakaojaribu kuzalisha vitakasa mikono feki mfanano wa hii.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...