Wednesday, April 1, 2020

Aliyekua Kaimu Mwenyekiti ACT Wazalendo akihama chama, amtolea povu Zitto Kabwe

KIMENUKA! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya aliyekua Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Yeremia Maganja kutangaza kukihama chama hicho kwa kile alichoeleza kutoridhishwa na mwenendo wa chama hicho.

Maganja ambaye pia amewahi kuwa mshauri wa ACT amesema sababu kuu zilizomfanya ajiondoe kwenye chama hicho ni namna ambavyo uchaguzi mkuu uliofanyika Machi mwaka huu ulivyoendeshwa pamoja na ujio wa Maalim Seif Sharif Hamad kutokea Chama cha Wananchi (CUF).

Amesema mwanzoni walivyoanzisha ACT ilikua ni kukitengeneza kuwa chama kinachofanya maamuzi yake kupitia vikao halali lakini matokeo yake kimekua chama cha mtu binafsi.

Akizungumzia uchaguzi mkuu uliofanyika katikati ya mwezi Machi, Maganja amesema haihitaji uchunguzi kujua kuwa uongozi wote uliochaguliwa ulikwishachaguliwa kabla ya mkutano mkuu uliowachagua.

" Uongozi wote mnaouona ulishachaguliwa kabla ya uchaguzi. Niwatapa mfano. Wapo watu waliochukua fomu za uongozi mbalimbali lakini wakajitoa siku ya uchaguzi na baadae wote wakateuliwa katika nafasi nyeti za Ujumbe wa Kamati Kuu.

Kuna wagombea walipigwa vita hadharani akiwemo mgombea wa Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ndugu Winston pamoja na ndugu Kaila. Walisakamwa hadharani kwamba hawafai kuwa viongozi.

Lakini hata Makamu Mwenyekiti aliechaguliwa bara, Ndugu Dorothy yeye alishinikizwa achukue fomu kugombea nafasi hiyo kwa kuwa ni Mwanamke na Mkristo. Sasa mtaweza kuona tupo kwenye chama cha namna gani," Amesema Maganja.

Amesema ujio wa Mwenyekiti wa ACT Taifa, Maalim Seif Sharif Hamad akitokea Chama cha Wananchi CUF kumesababisha mgawanyo ndani ya chama hicho kutokana na Maalim na watu wake kutaka kituo cha chama kiuongozi, kiuchumi na rasilimali watu kuwa Zanzibar.

Amesema Maalim Seif na watu wake wana ajenda yao na ACT ina ajenda yao na ajenda ya Maalim ni kuhakikisha chama hicho kinakua na nguvu Zanzibar kuliko bara.

" Siku moja Zitto aliweka picha yake akiwa Ubelgiji na Lissu na kusema wao ndo wanafaa kuwa marais wa Tanzania, nilicheka sana, Zitto anasukumwa na vitu viwili tu, maslahi binafsi na umaarufu. Hakuna kingine.

Niwaambie tu na nacheka moyoni, Zitto hafai kuwa kiongozi, atauza mpaka watu achilia mbali rasimali vitu, chama chetu kina matatizo na matatizo yetu ni Zitto Kabwe, huyu ndie huwa anapanga watu kwa wakati kwa maslahi yake binafsi na umaarufu wake," Amesema Maganja.

Akizungumzia muelekeo wake baada ya kuondoka ACT amesema amejipa siku kadhaa za kujitafakari ili kujua wanaenda chama gani ili waendelee kufanya siasa.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...