Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT-wazalendo, Zitto Kabwe amesema kuwa amemuandikia barua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuhusu janga la virusi vya Corona linalosambaa duniani hivi sasa.
Akisoma na kufafanua ujumbe huo katika mkutano na wanahabari Jijini Dar es Salaam, Zitto amesema kuwa yeye na chama chake wameamua kumuandikia barua Rais Magufuli kwakuwa janga hilo ni kubwa, hivyo kuna haja ya kushirikiana kwa pamoja na Serikali.
"Nimemuandikia barua rasmi mhe. Rais Magufuli kuhusiana na mapendekezo yangu na ya chama changu cha ACT wazalendo juu ya namna bora ya kudhibiti na kukabiliana na virusi vya Corona hapa nchini", amesema Zitto.
"Rais na Serikali yake wametangaza hatua za kupunguza kasi ya virusi hivi zikiwemo wananchi kujizuia na mikusanyiko isiyo ya lazima, kunawa mikono kwa maji safi yanayotiririka na sabuni pamoja na kuundwa kwa kamati 3 za baraza la mawaziri kuratibu mpango mzima. Hatua hizi ni za kupongezwa", ameongeza.
Kuhusu mapendekezo aliyoyatoa, Zitto amesisitiza umoja kwa Watanzania wote bila kujali itikadi ya chama, dini wala makabila, huku akimuomba Rais Magufuli kuanzisha kampeni ya kupima virusi vya Corona nchi nzima.
"Kama kuna jambo ninalolisisitiza kwa ukubwa wake basi ni kupima kupima kupima, lakini jambo lingine ni kuwepo kwa uwazi wa maambukizi mapya, wagonjwa mahututi na vifo vinavyotokana na ugonjwa huu. Nimemnasihi Mhe. Rais kwamba tusiongope kuwa wawazi kuhusu jambo hili kwa sababu uwazi una faida kubwa kuliko kuficha", amesema Zitto.