Na Ahmed Mahmoud Arusha
Mtu mmoja amefariki dunia Mara baada ya moto mkubwa kuzuka na kuunguza soko la Samunge jijini Arusha baada ya kufika na kushuhudia maduka yake yote yakiwa yameketea na moto.
Akiongea na waandishi wa habari Kaimu kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha amethibitisha kutokea kwa tukio hilo
Aidha wakati zoezi la kuzima moto likiendelea mtu mmoja aliyefahamika kwa majina ya James Peter Temba, 57 Mfanyabiashara na mkazi wa Moshono ambaye ni mmoja kati ya wamiliki wa vibanda vilivyoungua ndani ya Soko hilo, alifika eneo hilo na kukuta vibanda vyake vimeungua.
Kaimu kamanda Koka alieleza kuwa majira ya saa 23:30hrs, katika soko la Samunge, lililopo Mtaa wa NMC, kata ya Kati, Tarafa ya Themi, katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, moto ambao bado chanzo chake hakijajulikana uliwaka na kuteketeza vibanda vya Soko hilo ambavyo idadi na thamani yake bado haijajulikana.
Ameeleza kuwa vibanda hivyo vilikuwa vinamilikiwa na wafanyabiashara wa Soko hilo ambavyo vilijengwa kwa Mabati, Mbao na Mabanzi. Mara baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa hiyo kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Wananchi walifanikiwa kuzima moto huo ambao haukuleta madhara kwa binadamu.
Mtu huyo alipata mshtuko na kuanguka chini na kuzimia ambapo alichukuliwa na kupelekwa katika Hospital ya Mkoa ya Mount Meru na alifariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
Hata hivyo Uchunguzi unaendelea ili kubaini thamani halisi ya mali zilizoungua pamoja na chanzo cha moto huo.
Mwili wa Marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mount Meru kwa uchunguzi zaidi wa Daktari.
Natoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwa haraka pindi wanapoona majanga kama haya ya moto kwa Jeshi la Polisi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kudhibiti matukio kwa haraka kabla ya kuleta madhara makubwa.
Alitoa wito kwa wananchi na kuwaomba pamoja na wafanyabiashara kuwa watulivu wakati vyombo vya Ulinzi na Usalama vikifanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo halisi cha tukio hilo