Tuesday, March 24, 2020

CORONA: Bodaboda, bajaji zapigwa marufuku, minada nayo yazuiwa


Gavana wa Machakos nchini Kenya, Dkt. Alfred Mutua amezuia biashara ya bodaboda na bajaji katika kaunti hiyo ikiwa ni hatua za kupambana na kusambaa kwa virusi vya corona (Covid-19).

Kwa mujibu wa taarifa ya Gavana Mutua iliyotolewa leo, Machi 23, 2020 bodaboda na pikipiki hazitaruhusiwa kupakia abiria kwa kipindi cha wiki mbili kuanzia Jumatano, Machi 25, 2020.

"Kuanzia Jumatano, Machi 25 saa kumi na moja asubuhi, Bodaboda, Maruti au bajaji hazitaruhusiwa kufanya kazi katika Kaunti ya Machakos kwa kipindi cha wiki mbili. Kutogusana hakuwezekani wakati tunapanda bodaboda na umbali kati ya abiria na dereva ni zero hadi milimita 1," alisema Dkt. Mutua.

Hata hivyo, ili kuhakikisha anafidia sehemu ya hasara za kibiashara zinazotokana na zuio lake, alisema ameamua kusamehe kodi ya kipindi kilichobaki kwa mwaka 2020.

"Ili kufidia hasara, Serikali ya Machakos itasamehe kodi zote na ushuru wa Boadaboda, Maruti na Bajaji kwa kipindi chote kilichobaki hadi Desemba 31, 2020," aliongeza.

Aidha, aliongeza kuwa marufuku hiyo pia ni kwa minada iliyokuwa inafanyika katika maeneo mbalimbali, michezo na maeneo ya starehe za muziki (disco), akisisitza kuwa mkutano wa watu unaozidi watu watatu hautaruhisiwa katika kaunti hiyo.

Alisema kuwa pamoja na hatua hizo, maeneo yote ya masoko na kumbi yatapuliziwa dawa maalum ya kuua wadudu. Kenya ni moja kati ya nchi zilizoathirika na virusi vya corona (covid-19), na hadi sasa imeripoti visa 15.
Source
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...