Thursday, January 9, 2020

Gharama za Mafuta Zapanda Baada ya Shambulio la Iran


Gharama za mafuta zimepanda baada ya kambi mbili za majeshi ya Marekani nchini Iraq kushambuliwa na makombora.

Tokeo la picha la oil increase cost after iran attack

Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC, Gharama za mafuta ghafi zimepanda kwa 1.4% kwa dola 69.21 za Marekani kwa pipa moja. Wakati huo huo gharama za mafuta kwenye soko la dunia zilishuka kutokana na mzozo wa Mashariki ya kati.

Televisheni ya Taifa ya Iran ilisema kuwa shambulio lilikuwa ni kisasi baada ya kuuawa kwa kamanda wa juu wa jeshi la nchi hiyo Qasem Soleimani.

Shambulio lilitokea saa chache baada ya shughuli za mazishi ya Soleimani, aliyeuawa na shambulio la Marekani siku ya Ijumaa.

Kifo chake kilisababisha wasiwasi kuwa mzozo kati ya Marekani na Iran unaweza kuwa mkubwa zaidi.

Hali hii inaelezwa kuwa inaweza kuathiri usafirishaji wa mafuta kupitia lango la Hormuz linalotenganisha ghuba ya uajemi na ghuba ya Oman. Takribani moja ya tano ya mafuta duniani husafirishwa kupitia lango hilo linalounganisha eneo la ghuba na bahari ya Arabia.

Mlango wa Hormuz ni muhimu kwa wasafirishaji wakubwa wa mafuta katika eneo la ghuba – Saudi Arabia, Iraq, Umoja wa falme za kiarabu na Kuwait- ambao uchumi wao unajengwa kutokana na uzalishaji wa mafuta na gesi.

Iran pia inategemea kwa kiasi kikubwa njia hiyo kwa ajili ya kusafirisha mafuta. Qatar, mzalishaji mkubwa duniani wa gesi, husafirisha karibu gesi yake yote kupitia lango hilo.

Baada ya mashambulio, mamlaka ya anga ya Marekani imezuia ndege za Marekani kuruka kwenye anga ya Iraq, Iran na nchi jirani. Marufuku hiyo pia inahusisha ghuba ya Oman na maji ya kati ya Iran na Saudi Arabia.

Mamlaka hiyo imesema uamuzi umechukuliwa baada ya kuwepo kwa mvutano wa kisiasa na shughuli za kijeshi katika eneo hilo.

Kabla ya muongozo wa hivi karibuni, mamlaka hiyo ilishazuia ndege za Marekani kupaa umbali wa chini ya futi 26,000 katika anga la Iraq na kutopita kwenye eneo la anga ya Iran eneo la ghuba ya Oman tangu Iran ilipoidungua ndege isiyo na rubani ya Marekani mwezi Juni mwaka 2019.

Wakati huo huo shirika la ndege la Singapore limesema ndege zake zote hazitapita kwenye anga ya Iran.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...