Sunday, June 23, 2019

Waziri Lugola azidi kukomalia suala la Polisi na Bodaboda


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli kupitia ilani ya Chama Cha Mapinduzi iliyodhamiria kupambana na umaskini na changamoto ya ajira, Serikali ipo makini na wanahakikisha wananchi wanapambana na umaskini na tatizo la ajira.

Amesema hayo alipofanya ziara ya kushtukiza katika Kituo cha Polisi Gogoni kilichopo Wilaya ya Kipolisi Kimara, Wilayani Ubungo, jijini Dar es Salaam, leo kwa lengo la kuangalia utendaji wa Polisi kituoni hapo.

Aidha, amesema vijana wengi wameamua kupambana na umaskini kwa kujiajili kupitia pikipiki maarufu bodaboda lakini kumekuwa na malalamiko mengi ambayo yalifika hadi bungeni kwa vijana hao kuonewa, kupigwa na kunyang'anywa pikipiki zao.

"Nilitoa maagizo kwa Jeshi la Polisi juu ya bodaboda ambazo zinaweza kukamatwa na kuwekwa katika vituo vya polisi; bodaboda  zinazostahili kukamatwa ni zile zilizohusika na uharifu, zilizohusika na ajali, zilizopotea na kuonekana na zile zilizookotwa," alisema Lugola.

Aliongeza kuwa, bodaboda nyingine zinazokamatwa na makosa mengine ya usalama barabarani kwa kupakia abiria zaidi ya mmoja maarufu kama mshikaki na kutovaa kofia ngumu na mshtakiwa anaweza kutozwa faini ambayo italipwa ndani ya siku saba.

Hata hivyo, Waziri Lugola baada ya ziara yake hiyo ambapo alizikagua bodaboda mbalimbali kituoni hapo, alisema amejiridhisha kwa kukuta bodaboda zote zipo kwenye makundi aliyoyaainisha na amelipongeza na amempongeza Mkuu wa Jeshi hilo, Simon Sirro kwa maelekezo yake aliyoyatoa kwa Jeshi hilo kufanyiwa kazi.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...