Saturday, March 23, 2019

Serikali yaongeza vifaa tiba ili kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini


Serikali imeendelea kuboresha huduma za matibabu ya kifua Kikuu kwa kuongeza vituo vya kutolea huduma za matibabu sambamba na kuongeza vifaa tiba, ikiwa ni jitihada za Serikali kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) nchini.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu leo wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za kifua Kikuu na kutoa tamko kuhusiana na ugonjwa huo katika Hospitali ya Mbagala Jijini Dar es salaam.


"Huduma za matibabu ya Kifua Kikuu (TB) sugu zimesogezwa karibu kwa wananchi, ambapo kwa sasa tunazo hospitali 93 za kutibu Kifua Kikuu sugu ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo, huduma za matibabu zilikuwa zinapatikana katika Hospitali ya Kibong'oto pekee " amesema Waziri Ummy.

Pia, Waziri Ummy amesema katika kila Watanzania 100,000 Watanzania 269 wanahisiwa kuwa na ugonjwa wa Kifua Kikuu, huku watu 70 wanafariki kila siku kutokana ugonjwa wa Kifua Kikuu ambapo ni sawa na watu watatu hufariki kila saa. "watu 70 kila siku kutokana na ugonjwa wa Kifua Kikuu, kwahiyo kila saa ni sawa na watu watatu wanafariki kutokana na ugonjwa wa Kifua Kikuu ambao unatibika " alisema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema takribani wagonjwa 154,000 wanaokadiriwa kuugua ugonjwa wa Kifua Kikuu wanapaswa kufikiwa na kuingizwa katika mpango wa matibabu kila mwaka ili kuutokomeza ugonjwa huu nchini.

Waziri Ummy ameendelea kusema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 Duniani zenye kiwango kikubwa cha wagonjwa wa Kifua Kikuu, inakadiriwa kuwa wapo wagonjwa takribani 154,000 ambao huugua ugonjwa wa kifua Kikuu kila mwaka.

Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa Mgonjwa wa Kifua Kikuu ambae hajaanza matibabu anaweza kuambkiza Kati ya watu kumi hadi watu 20 kwa mwaka, hivyo jitihada za makusudi zinatakiwa kuendelea kuchukuliwa ili kutokomeza ugonjwa huu nchini.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...