Kumeshuhudiwa kioja katika kijiji cha Shimanyiro eneo bunge la Ikolomani Kaunti ya Kakamega nchini Kenya baada ya nyumba ya mama mmoja kuteketezwa kwa moto na wanaodaiwa kuwa ni majini/mapepo.
Kisa hicho kilichotokea usiku wa kuamkia Jumanne, Februari 19,2019 kimewaacha wakazi na mushtuko mkubwa huku Electine Mushila (36) akilazimika kulala nje na mtoto wake mchanga baada ya nyumba kuteketea kwa moto juu ya paa pekee huku vitu ndani ya nyumba vikiwa haviungui.
Mwanamke huyo alipaswa kurithi ushirikina huo kutoka kwa mama mkwe lakini alikataa na anasema mapepo wamekuwa wakimbeba mwanawe wa miezi 11 nyakati za usiku na kumpeleka mtoni.
Inaelezwa kuwa masaibu ya Electine yalianza pale alipokataa kurithi ushirikina kutoka kwa mama mkwe, kanuni ambazo zimekuwa zikifuatwa na familia hiyo.
Anasema kuwa, mama mkwe alikasirishwa na hatua ya mke wa mtoto wake kukataa kushiriki ushirikina na ndipo sasa akaamua kumteremshia mapepo ambao wamekuwa wakimtaabisha mara kwa mara.
Mama mkwe huyo anadaiwa kushusha moto na kuunguza nyumba aliyokuwa analala mwanamke huyo.
Mbali na kuteketeza nyumba, mapepo hao wamekuwa wakimbeba mwanawe wa miezi mitano nyakati za usiku na kumpeleka mtoni jambo ambalo limesababisha familia yake akiwamo mamake (Jane Mushila) kumtoroka.
"Tumeshtuka kuona moto ukiwaka na kuchoma paa la nyumba. La kushangaza vitu vilivyokuwa ndani ya nyumba hiyo havikuwa vinateketea. Si mara ya kwanza kwa mambo kama haya kutendeka kuna nyakati zingine ambapo mapepo hawa wamekuwa wakimbeba mtoto wake na kumpeleka mtoni," alisema mmoja wa jirani zake.
Hata hivyo, wakazi wa eneo hilo wakiongozwa na Benard Ngosinge wamemtaka mume wa Electine kufanya sherehe za tambiko ili kuzuia mapepo ambao huenda wametumwa kwake kutawala.
"Ningemwomba kijana wangu Felix, kama kuna chochote ambacho umekipanda ama unacho katika boma lako kinachohusiana na ushirikina kama vile nilivyoambiwa na mke wako, nakusihi uje utoe na tufanye sherehe ya tambiko itakayokukinga wewe pamoja na familia yako dhidi ya mapepo," Ngosinge alisema.
Kwa upande mwingine mama wa Electine anailaumu familia alikoolewa binti yake huku akitishia kumchukulia hatua za kisheria mume wa mwanawe.
"Hatuwezi ishi na watu kama hawa katika eneo hili. Mume wa familia hiyo hajakuwa akiishi hapa na si mzaliwa wa eneo hili.
Tunashuku alitimuliwa alikokuwa na hivyo akaja huku kujificha na mapepo yake," alisema mkazi mwingine.
Wakati uo huo, kaimu chifu wa eneo hilo Caleb Murunga amepuuzilia mbali uwepo wa ushirikina sehemu hiyo na kuwataka wenyeji kuwa watulivu huku uchunguzi wa kina ukianzishwa.