Mbunge wa Viti Maalum, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kunti Yusuf Majala, amejeruhiwa vibaya baada ya gari alilokuwa akisafiria kupata ajali. Anaripoti Yusuph Katimba.
Ajali hiyo imetokea leo Jumatatu, tarehe 24 Desemba, maeneo ya Kilema, katikati ya wilaya za Chemba na Kondoa.
Taarifa zilizothibitishwa na ofisa mmoja wa Bunge mjini Dodoma, ambaye hata hivyo, hakupenda kutajwa jina lake, zinaeleza kuwa katika ajali hiyo, watu wengine wanne wamefariki dunia.
Afisa huyo ambaye anasema siyo msemaji wa Bunge, anaeleza kuwa gari ambalo mbunge alikuwa akilitumia lilianguka baada ya kuchomoka tairi la mbele mkono wa kushoto wa dereva.
Anasema, "gari hili lilikuwa na watu 11 (kumi na moja), watoto saba na wakubwa wanne. Mhe. Kunti ana maumivu makali sana ya kiuno na shingo."
Anasema, kufuatia hali ya mbunge huyo kuwa mbaya, ofisi ya Spika, imeanza kufanya utaratibu wa haraka wa kuhakikisha mara atakapofikishwa kwenye hospitali ya mkoa wa Dodoma, aweze kusafirishwa yeye na majeruhi wengine, kupelekwa jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi."
Hata hivyo, afisa huyo hakuweza kuwafahamu mara moja majina ya wale waliofariki dunia; na au kujeruhiwa. Bali, taarifa kutoka maofisa wa Chadema zinasema, baadhi yao waliofariki, sehemu kubwa watakuwa familia ya mbunge huyo.
Kwa mashuhuda, gari lililokuwa limembeba Kunti na ambalo limepata ajali, lilikuwa na namba za usajili, T 624 DPE. Lilikuwa likitokea Dodoma mjini kuelekea Kondoa.
Dereva wa gari hilo alikuwa ni Stephano Masawe, ambaye ni dereva wa Katibu wa Chadema, Kanda ya Kati.
Chanzo - Mwanahalisi online