Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amekataa masharti yaliyotolewa na kada wa chama hicho, Bernad Membe katika ujumbe wake kupitia kitandao ya kijamii na kusema huo siyo utaratibu wa kukutana na wanachama wake.
Dk Bashiru amesema hayo jana Jumamosi Desemba 1, 2018 wakati akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM wilaya ya Bukombe mkoani Geita.
Amesema katika miaka 10 iliyopita CCM haikufanya vizuri kutokana kikundi cha wachache kujifanya ndiyo wenye nguvu na kudharau jambo lililosababisha chama kisipendwe na wapiga kura.
Amesema tangu achaguliwe kuwa katibu mkuu hajawahi kuonana na Membe na licha ya chaguzi zote zinazofanyika za kurudisha wabunge, Membe aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nje hajawahi kutoa mchango wowote wa mawazo.
Amesema Membe kama mwanachama mwingine hana nguvu zaidi ya chama hivyo bado anamhitaji afike kwake bila masharti yoyote.
"Sikumsema Membe kama mtu maarufu au mwenye nguvu bali nimemsema kama mwanachama wa kawaida, hana tofauti kabisa na wanachama walioingia leo, ila ana tofauti kwa kuwa amekuwa waziri na mbunge" amesema Dk Bashiru
"Namuhitaji sana (Membe), ningekuwa na namba yake ya simu ningempigia," ameongeza.
Amesema CCM kipindi cha nyuma imeumizwa na makundi, fitina, uongo na nguvu ya pesa mambo ambayo sasa hawapo tayari kuyaendeleza.
Dk Bashiru ametoa kauli hiyo kujibu ujumbe unaodaiwa kuwa wa Membe aliyeutoa kupitia mitandao ya kijamii akijibu wito wa katibu mkuu huyo wa CCM kumtaka kufika ofisini kwake kujibu tuhuma zinazodaiwa kutaka kumkwamisha Rais John Magufuli.
Katika ujumbe huo ulioandikwa na mtu aliyejiita Bernard Membe unasema; Kufuatia taarifa za kwenye mitandao jioni (jana) hii na ujumbe mfupi unaotumwa kwake "Nimeamua kutoa ujumbe huu kwa wote wanaonitakia mema."
"Usiku huu nimempelekea Katibu Mkuu wa chama chetu ndugu Bashiru ujumbe wa kukubali kumwona mara nitakaporejea kutoka nje ya nchi."
"Nimeshangazwa kidogo na utaratibu uliotumika kuniita, lakini kwa sababu ya ugeni kazini na kwa sababu ninamheshimu, nitakwenda kumwona ofisini kwake," amesema.