Baraza la Sanaa Taifa, (BASATA) Julai 26, 2018 lilimzuia msanii wa muziki, Diamond Platnumz kwenda kufanya show nje ya nchi akiwa katika uwanja wa Mwl. JK Nyerere jijini Dar es salaam huku likieleza sababu kuwa hakuwa na kibali kutoka kwao cha kwenda kufanya show nje ya nchi.
Akielezea sakata hilo Katibu Mtendaji wa BASATA, Godfrey Mngereza amesema kuwa kwa sasa kuna utaratibu mpya ambao msanii akitaka kwenda kufanya show nje ya nchi ni lazima apitie BASATA wampe kibali na kisha akirudi pia anatakiwa kuripoti kwao.
BASATA wamesema wamemzuia Diamond ili liwe fundisho kwa wasanii wengine ambao wanamazoea ya kwenda nje ya nchi kufanya matamasha bila kila kibali kutoka kwao.
“Utaratibu wa msanii kuwa na kibali anapoenda nje, yaani kutambua wapi anaelekea kikazi si mpya. Upo katika kanuni toka awali. Lengo ni kumhakikisha ulinzi wa haki na usalama wake pale kutakapotokea suala lisilo rafiki. Pia, kumuaga kwa kukabidhi bendera na mapokezi pindi anaporudi ikibidi,“amesema Mngereza kwenye mahojiano yake na TBC na kusisitiza kwanini wamemchukulia Diamond hatua hiyo.
“Tumefanya hivi ili liwe fundisho kwa wasanii wetu wengine ambao bado wanakiuka jambo hili, wasanii wetu wanapoandaa vitu vya kwenda navyo vya kwenda kuonesha show nje ya nchi pale wanapoandaa tamasha. Tunawaasa wapitie taratibu, Kanuni na sheria za BASATA wala sio ngumu kiasi hicho.“amemaliza Mngereza.
Hata hivyo, Diamond Platnumz na timu yake alifanikiwa kuondoka nchini jana usiku na anatarajiwa kesho kutumbuiza katika visiwa vya Mayotte nchini Ufaransa.
The post BASATA watema cheche baada ya kumzuia Diamond kusafiri nje ya nchi ‘tumefanya kwake liwe fundisho kwa wengine’ appeared first on Bongo5.com.Source