Saturday, August 29, 2026

NDEJEMBI AAPISHWA IKULU! RAIS SAMIA ASEMA 'NAFASI IMEKABIDHIWA KWA KIJANA KAWATUMIKIE WATANZANIA BILA KUJALI TOFAUTI ZAO'

 Na Janeth Raphael - MichuziTv -Ikulu Chamwino


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema uamuzi wa kumteua Deogratius Ndejembi kuwa Makamu wa Rais ulizingatia sifa, uzoefu na uwezo wake wa kubeba dhamana kubwa ya uongozi wa taifa.

Rais Samia amesema nafasi hiyo imekabidhiwa tena kwa kijana, akimtaka Ndejembi kutumia fursa hiyo kujifunza, kukua kiakili na kutekeleza majukumu yake kwa weledi, utii na uaminifu kwa maslahi ya Watanzania.

Akizungumza leo, Agosti 29, 2026, katika hafla ya kumuapisha Ndejembi kuwa Makamu wa Rais iliyofanyika Ikulu Chamwino, Dodoma, Rais Samia amesema uamuzi wa kumrudisha kijana katika nafasi hiyo ulifanyika kwa kauli moja.

“Kwa kauli moja tuliamua kuirudisha nafasi ya Makamu wa Rais kwa vijana na tuendelee kulea. Imetoka kwa kijana na tumeirudisha kwa kijana. Tunakuomba kijana (Ndejembi) ukakue sio kwa umri bali ukakue kiakili, tumekupa majukumu makubwa ni imani yangu utaweza,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema Ndejembi alipata uungwaji mkono wa wabunge kwa kauli moja kutokana na sifa alizonazo zinazomfanya astahili kushika nafasi hiyo.

“Wabunge walimpitisha Deogratius Ndejembi kwa kauli moja kwa kuzingatia sifa za Makamu wetu wa Rais,” amesema.

Amesema kabla ya kufikia nafasi ya Makamu wa Rais, Ndejembi amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini na katika sekta binafsi, akieleza kuwa uzoefu huo utakuwa nyenzo muhimu katika utekelezaji wa majukumu yake mapya.

“Makamu wa Rais Deogratius Ndejembi, kabla ya wadhifa huu, ulishika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini na sekta binafsi. Sina shaka kwamba uzoefu huo utakusaidia kutekeleza majukumu ya dhamana hii uliyopewa,” amesema Rais Samia.

Kwa mujibu wa Rais Samia, hakuna shule maalumu inayomwandaa mtu kuwa Makamu wa Rais, bali uwezo wa kutekeleza majukumu hayo unajengwa kupitia sifa binafsi, bidii, weledi, nidhamu pamoja na utayari wa kujifunza na kusimamia utekelezaji wa majukumu.

Amesema sifa hizo zitamsaidia Ndejembi kutekeleza ipasavyo dhamana aliyopewa na taifa.

Rais Samia pia amesema uzoefu wa Ndejembi ndio uliowafanya viongozi kutokuwa na kusita katika kupitisha jina lake wakati wa kutafuta mtu wa kujaza nafasi hiyo.

“Kwa uzoefu huo ndio maana wakati tunatafuta mtu wa kujaza nafasi hii, hatukusita hata kidogo kupitisha jina lako. Hivyo ni matamanio na matarajio yetu sote Watanzania utalitumikia vyema, kwa utii, uaminifu, utu, busara, uzalendo, hekima, maarifa na uzoefu ulio nao, ukimtanguliza Mungu mbele na kwa maslahi ya taifa,” amesema.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amemtaka Ndejembi kwenda kuwatumikia Watanzania wote bila kujali tofauti zao, akisisitiza umuhimu wa kiongozi kuweka mbele maslahi ya taifa.

“Nenda ukawatumikie Watanzania bila kujali tofauti zao,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema serikali ina kazi kubwa ya kutekeleza ahadi zilizowekwa kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030, sambamba na kuanza utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya miaka 25 ijayo.

Amesema dira hiyo imebeba matarajio makubwa ya maendeleo kwa wananchi, hivyo utekelezaji wake unahitaji umoja, mshikamano, ushirikiano, utulivu na uongozi bora.

“Ili tuweze kutekeleza haya yote kwa maslahi ya wananchi wetu na taifa kwa ujumla, tunahitaji umoja, mshikamano, ushirikiano, utulivu na uongozi bora,” amesema.

Uapisho wa Ndejembi unafungua rasmi ukurasa mpya katika safari yake ya uongozi wa kitaifa, huku akianza kutekeleza majukumu ya Makamu wa Rais chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan
















Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...