Meneja wa mfuko wa bima ya Afya Mkoa wa Ruvuma Hansi John Akizungumza na waandishi wa habari waliomtembelea ofisini kwake kuhusu mipango ya serikali kuzifikia kaya zisizo na uwezo na utekelezaji wake kwa awamu kupitia mpango wa TASAF.
Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Mfuko wa Bima ya Afya Mkoa wa Ruvuma umefanikiwa kuwafikia zaidi ya wanufaika 17,000 kutoka kaya zisizo na uwezo katika utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unaotekelezwa na Serikali kupitia mpango wa TASAF.
Meneja wa Mfuko wa Bima ya Afya Mkoa wa Ruvuma, Hansi John, amesema Serikali ilitoa nafasi ya kusajili zaidi ya kaya 11,000 mkoani humo na hadi sasa asilimia 53 ya kaya hizo zimefikiwa huku zoezi likiendelea katika wilaya zote za mkoa huo.
Akizungumza ofisini kwake, Hansi amesema changamoto ya wakazi wengi wa Ruvuma kuwa mashambani katika shughuli za kilimo ilisababisha baadhi ya walengwa kushindwa kufikiwa kwa wakati, lakini sasa wananchi wengi wameanza kurejea vijijini jambo litakalowezesha kukamilika kwa usajili wa asilimia 46 zilizobaki.
Amefafanua kuwa Serikali tayari imegharamia gharama zote za bima kwa kaya hizo ili kuhakikisha wananchi wasiokuwa na uwezo wanapata huduma za afya bila vikwazo vya kifedha.
Kwa mujibu wa meneja huyo, kaya zinazonufaika hutambuliwa kupitia mikutano ya vijiji ambapo wananchi hupiga kura kuwabaini wale wasiokuwa na uwezo wa kuchangia huduma za afya.
Orodha hizo hupitiwa na maafisa ustawi wa jamii kwa kushirikiana na ofisi za TASAF katika halmashauri husika kabla ya kuwasilishwa kupitia TAMISEMI kwa ajili ya usajili rasmi katika mfumo wa bima ya afya.
Hansi ametoa wito kwa viongozi wa kata, vijiji, wazee maarufu pamoja na wananchi walioteuliwa kujitokeza pindi wanapopata taarifa za usajili ili kuepusha matumizi yasiyo ya lazima ya rasilimali katika kuwatafuta walengwa.
Amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na bima ya afya ili kupata huduma stahiki na kuchangia maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla.
Meneja wa mfuko wa bima ya Afya Mkoa wa Ruvuma Hansi John akiwa ofisini kwake katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.