Chama wa wafanyakazi wakatoliki CWM kinaendelea na mchakato wa kutoa semina kwa wanawake wa makundi mbali ili kupaza sauti kwa jamii kutambua thamani,wajibu na haki za wafanyakazi wa majumbani
Mkakati wa kuyafikia makundi hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maono na misingi ya Chama hicho kuwa sauti kwa wasio na sauti hasa wafanyakazi wa majumbani ambao katika utekelezaji wa majukumu yao hukutana na vikwazo mbalimbali
Aidha leo June 5 CWM imekutanisha kundi la wanawake wakatoliki na makundi mengine ya wanawake katika parokia ya Teule ya Mtakatifu Benedict Mkundi Jimboni Morogoro
Miongoni mwa mambo yanayojadiliwa katika mafunzo hayo ni kukazia mchakato wa uwepo wa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wa majumbani, haki na wajibu wao kama zilivyo kazi nyingine
EDSON YEYEYE ni Mratibu CWM Taifa,amewaagiza washiriki hao kuimarisha malezi ya kimaadili kwa wafanyakazi hao, ili kulinda heshima na utu wa Mfanyakazi wa nyumbani.
Kwa upande wake Frola Ng'eni Katibu wa CHODAWU mkoa wa Morogoro amesema mfanyakazi ana haki ya kushikishwa kujiunga na mfuko wa jamii,Nssf kwa ajili ya akiba yake ya baadaye.
Hata hivyo amesema kuwa sekta ya wafanyakazi wa majumbani ni sekta muhimu katika kukuza pato la familia na taifa, hivyo wanatakiwa kupewa haki wanazostahili bila kunyanyaswa
CWM inalenga kuyafikia makundi mengi ya wanawake Jimboni Morogoro ambapo hivi karibuni wanatarajia kukutana na kundi la wafanyakazi wa Majumbani ili kukamilisha mkakati wa kuwapeleka katika mafunzo ya ufundi stadi katika chuo cha Veta Mikumi
