Rais wa Jamhuri ya Kenya, William Ruto, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuunda Tume ya Jaji Othman Chande kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Ruto ametoa pongezi hizo alipowasili nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi, akieleza kuwa hatua hiyo ni ishara ya uongozi makini na wenye kuwajibika katika kushughulikia changamoto za kitaifa kwa njia ya kisheria na kiutawala.
Amesema kuundwa kwa tume hiyo kunaonesha dhamira ya Serikali ya Tanzania katika kutafuta ukweli wa kilichotokea na kuhakikisha masuala yote yanayohusu amani na utulivu yanapatiwa ufumbuzi wa kudumu ndani ya mipaka ya nchi.
Kwa mujibu wa Rais Ruto, juhudi hizo zinaungwa mkono na nchi za Afrika Mashariki, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa kikanda kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa ukanda huo.
Ameongeza kuwa kutokana na uzoefu wa Kenya katika nyakati kama hizo, ana imani Tanzania itaweza kupitia kipindi hicho na kuibuka imara zaidi, huku akiahidi ushirikiano na nia njema katika kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa.
Tume ya Jaji Othman Chande iliundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa TanzaniaDkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi huo, ikiwa ni sehemu ya hatua za kuimarisha utawala bora na kudumisha amani nchini.
