Daktari wa mifugo Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma Dkt Seria Masole akizungumzia umuhimu wa kujiajiri badala ya kusubiri qjira katika kongamano la vijana leo ukumbi wa Manispaa ya Songea
Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Mkuu wa Wilaya ya Songea, Kapenjama Ndile, amewataka vijana nchini kuwa wazalendo na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa huku wakiepuka vitendo vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Ndile ametoa wito huo leo Mei 13, 2026 wakati akizindua Kongamano la Vijana kuelekea Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, zinazotarajiwa kuwasili katika Manispaa ya Songea Mei 18 mwaka huu.
Kongamano hilo limefanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma likiwakutanisha vijana pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali na chama.
Katika kongamano hilo, vijana wamepata nafasi ya kushiriki mijadala mbalimbali kwa kuuliza maswali na kujibiwa na wawezeshaji waliokuwa ukumbini hapo.
Mafunzo yaliyotolewa yamehusu afya ya akili, ujasiriamali, maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na UKIMWI, pamoja na elimu ya uraia na uzalendo iliyotolewa na maafisa kutoka idara mbalimbali ikiwemo uhamiaji.
Wawezeshaji hao wamesisitiza umuhimu wa vijana kutumia elimu hiyo kujiletea maendeleo binafsi na ya jamii inayowazunguka.
Aidha, kongamano hilo lililenga kuwaunganisha vijana ili waweze kutambua na kutumia fursa za kiuchumi zinazopatikana katika maeneo yao kwa ajili ya kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.
Vilevile, vijana wamepatiwa elimu ya kujikinga dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya, rushwa pamoja na vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo vimekuwa changamoto kwa jamii.
Washiriki wa kongamano hilo wameeleza kuwa mafunzo hayo yamewapa mwanga mpya wa namna ya kushiriki katika shughuli za maendeleo na kulinda maadili ya taifa.
Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 zinatarajiwa kuwa sehemu ya kuhamasisha maendeleo na mshikamano wa wananchi katika Manispaa ya Songea, huku viongozi wakitumia jukwaa hilo kuendelea kuwahimiza vijana kuwa chachu ya maendeleo, amani na uzalendo nchini.
Kongamano hilo limeonekana kuwa mwanzo mzuri wa maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru kwa kuwajengea vijana uelewa na hamasa ya kushiriki katika shughuli za kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya taifa.





