Benki ya CRDB imeendelea kuwazawadia wateja wake kwa zawadi nono kupitia promosheni maalum ya matumizi ya kadi ya TemboCard Visa, huku zawadi kubwa ikiwa ni safari ya kwenda Marekani kushuhudia fainali za Kombe la Dunia 2026.
Zawadi hizo zimekabidhiwa Aprili 14, 2026 katika hafla iliyofanyika makao makuu ya benki hiyo yaliyopo Upanga, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali nchini.
Kupitia kampeni hiyo, wateja wanahimizwa kutumia TemboCard Visa katika malipo yao ya kila siku kupitia mashine za POS au mtandaoni, ambapo kila muamala unaongeza nafasi ya kushiriki katika droo mbalimbali za ushindi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja Mwandamizi wa Kitengo cha Kadi (Card), Karington Chahe, amesema lengo la kampeni hiyo ni kuwapa wateja fursa ya kipekee ya kushinda zawadi kubwa huku wakinufaika na huduma salama, rahisi na za kisasa.
Ameeleza kuwa droo ya kwanza tayari imefanyika na kutoa washindi kadhaa waliopata zawadi mbalimbali ikiwemo runinga janja (Smart TV) za inchi 80 pamoja na vifurushi vya DSTV kwa washindi watatu.
Chahe amebainisha kuwa zawadi ya kilele katika kampeni hiyo ni tiketi nne kwa Watanzania kusafiri kwenda Marekani kushuhudia mashindano ya Kombe la Dunia 2026, yatakayowakutanisha mastaa wakubwa wa soka duniani kama Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.
“Tunawahimiza wateja wetu kuendelea kutumia kadi zao katika malipo ya kila siku ili kuongeza nafasi ya kushinda zawadi hizi adhimu, ikiwemo safari ya kwenda kushuhudia Kombe la Dunia,” amesema Chahe.
Kampeni hiyo ilizinduliwa rasmi Machi 12, 2026, ikiwa na lengo la kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya malipo ya kidijitali pamoja na kuwazawadia wateja kwa uaminifu wao kwa benki hiyo.
Kwa mujibu wa Benki ya CRDB, hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wake wa kuendeleza ubunifu katika huduma za kifedha, huku ikiwahamasisha Watanzania kupunguza matumizi ya fedha taslimu na kuhamia katika mifumo ya kisasa iliyo salama na yenye ufanisi.
