Tuesday, March 24, 2026

DUNIA YAIPIGIA SALUTE TANZANIA: TUZO ZA STANBIC JIJINI LONDON NI JIBU KWA WANAOBWABWAJA MITANDAONI



Wakati baadhi ya watu wakitumia muda wao kwenye mitandao ya kijamii kubwabwaja na kupotosha kuwa uchumi wa Tanzania unayumba, jumuiya ya kimataifa imetoa jibu la kishindo kupitia sekta ya fedha. Tuzo tatu za kimataifa alizotunukiwa Mtendaji Mkuu wa Stanbic Tanzania, Manzi Rwegasira, jijini London nchini Uingereza, ni kielelezo tosha kuwa mfumo wetu wa kifedha uko imara na unaheshimika duniani.

Jarida la Euromoney, ambalo ni mamlaka ya juu ya tathmini ya kibenki duniani, haliwezi kuipa Benki ya Stanbic tuzo ya Benki Bora ya Kimataifa kwa mwaka wa pili mfululizo kama mazingira ya biashara na usalama wa shilingi yetu yangekuwa shakani. Hii ni tafsiri ya wazi kuwa Tanzania ina watu wenye akili na weledi wanaosimamia misingi ya fedha, na si kama inavyochorwa na "wapiga kelele" wa kidijitali.

Ushindi huu ni salamu kwa wawekezaji kuwa shilingi ya Tanzania na mfumo wake wa kibenki ni sehemu salama ya kuweka na kukuza mali. Kitendo cha Stanbic kutajwa kuwa Benki Bora ya Kimataifa kwa Wateja Maalumu (Private Banking) kinaonyesha uwezo wa kipekee wa kuunganisha uchumi wa ndani na masoko ya dunia.

Hii ina maana kuwa, licha ya changamoto za kiuchumi zinazoikumba dunia kwa sasa, Tanzania imefanikiwa kujenga "daraja la kifedha" linalowawezesha wateja kukuza mali zao nje ya mipaka kwa usalama. Heshima hii tuliyoipata jijini London inathibitisha kuwa sera zetu za kifedha zinaaminika na majopo huru ya wataalamu wa kimataifa, jambo linalowapa imani washirika wa maendeleo na wafanyabiashara wakubwa duniani.

Aidha, Tuzo ya Benki Bora kwa Kizazi Kijacho iliyonyakuliwa na Stanbic ni ujumbe mzito kwa mustakabali wa biashara za Kitanzania kuelekea Dira ya 2050. Hii inaashiria kuwa kuna maandalizi ya dhati ya kuwavusha warithi wa mali na vijana kusimamia uchumi kwa uwajibikaji.

Tunapoona taasisi zetu zikishinda tuzo za namna hii, tafsiri yake ni kwamba uchumi wetu haujajengwa kwa kubahatisha, bali kwa mikakati inayolenga uendelevu wa vizazi. Ni uthibitisho kuwa Tanzania inapiga hatua kubwa katika namna mali zinavyoundwa na kusimamiwa, ikijitofautisha na mataifa mengine yanayokumbwa na migogoro ya usimamizi wa rasilimali.

Kwa upande wa huduma kwa wateja, tuzo hiyo ya tatu inashindilia msumari kwenye ukweli kwamba mabenki yetu yameacha kufanya kazi kama ofisi za kutoa fedha tu, bali yamekuwa washauri wa kimkakati wa maamuzi ya kifedha. Huu ni ushindi wa kila Mtanzania anayeamini katika maendeleo ya nchi yake.

Hii inatupa picha kuwa Tanzania ipo sawa na mataifa mengine makubwa duniani katika kutoa huduma za kiwango cha juu. Hivyo, badala ya kusikiliza upotoshaji wa mitandaoni unaodai "Tanzania haiwezekani," tuzo hizi za Euromoney Private Banking Awards 2026 ni kioo kinachoonyesha kuwa Tanzania inawezekana na inasonga mbele kwa kasi ya ajabu katika anga za kimataifa.

Mafanikio haya ya Stanbic Tanzania ni heshima kwa nchi na ni kigezo cha tathmini kuwa uchumi wetu unaenda vyema chini ya usimamizi makini.

Tunapokuwa na benki zinazong'ara London, maana yake ni kwamba soko letu la fedha limekomaa na lina ushindani unaohitajika kuvuta mitaji mipya. Ni wakati wa Watanzania, hasa vijana, kuacha kuyumbishwa na maneno ya mitandaoni na badala yake waone fahari na fursa zilizopo katika mfumo wetu wa kifedha uliopata baraka za dunia. Tanzania inaheshimika, shilingi yetu inalindwa na weledi, na mustakabali wa mali za Watanzania upo katika mikono salama na ya kisasa.





Labels:Habari



SHARE:








COMMENTSBLOGGERFACEBOOK: DISQUS





WEEK TRENDING

Monday, March 23, 2026

MIRADI YA SHILINGI BILIONI 85 KUCHOCHEA USHIRIKIANO WA TANZANIA NA AUSTRIA


Tanzania na Austria zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati yenye thamani ya Euro milioni 30 (takriban Shilingi bilioni 85), itakayolenga sekta za elimu, usalama na ufundi.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Munde, Machi 23, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa mazungumzo na ujumbe kutoka Austria ulioongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria anayeshughulikia masuala ya kisiasa, Mhe. Balozi Dkt. Hannah Liko. Amesema ziara hiyo imekuja wakati muafaka ambapo Tanzania inahitimisha Dira ya Maendeleo ya 2025 na kuanza mchakato wa Dira mpya ya 2050.

Mhe. Munde amebainisha kuwa Austria imekuwa ikifadhili miradi muhimu kupitia mikopo nafuu inayochangia moja kwa moja maendeleo ya wananchi, ikiwemo mradi wa ukarabati na uwekaji wa mifumo ya kisasa katika Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Karume (KIST) Zanzibar pamoja na maboresho ya mfumo wa elimu visiwani humo. Miradi mingine ni ukarabati wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) pamoja na ununuzi na usambazaji wa magari ya kuzima moto na vifaa vya uokoaji Zanzibar.

Aidha, Mhe. Munde amewasilisha salamu za shukrani kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa Austria ni mshirika wa maendeleo anayeaminika na kwamba Tanzania iko tayari kuimarisha ushirikiano huo kwa lengo la kuinua hali ya kijamii na kiuchumi ya wananchi.

Kwa upande wake, Balozi Dkt. Liko amepongeza ushirikiano huo madhubuti na kuahidi kuwa Austria itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta za utalii na viwanda ili kuongeza tija ya kiuchumi kwa pande zote mbili.

Katika mazungumzo hayo, pande zote mbili pia zimejadili utekelezaji wa Mkakati wa Austria na Afrika wa mwaka 2026–2029 unaolenga kuimarisha amani na usalama, kukuza uchumi wa kijani, kukabiliana na uhamiaji haramu huku ikiimarishwa mifumo ya uhamiaji wa kisheria na wenye tija, pamoja na kuendeleza sayansi na elimu.

Sunday, March 22, 2026

Mwili wa mwanaume waokotwa Magugu, wananchi waishi kwa hofu.


Na John Walter-Babati

Tukio la kusikitisha limeutikisa wakazi wa eneo la Magugu, wilayani Babati mkoani Manyara, baada ya mwili wa mwanaume ambaye bado hajatambulika kukutwa umetupwa pembeni mwa barabara kuu ya Babati–Arusha.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, marehemu ana dalili za kuuawa kikatili, huku chanzo cha tukio hilo kikiwa bado hakijabainika.

Wananchi wa eneo hilo wameeleza hofu kubwa kufuatia tukio hilo, wakihofia usalama wao na kuziomba mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kuwabaini wahusika na kuimarisha ulinzi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Magugu, Lohay Amos, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, akieleza kuwa limetokea usiku wa kuamkia Machi 19 katika eneo la Kwa Chami.

Amesema mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa na majeraha makubwa kichwani, ambapo inaelezwa kuwa alipigwa na kitu kizito kinachofanana na shoka, hali iliyosababisha kuharibika kwa taswira ya uso na kufanya kuwa vigumu kutambulika.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya Magugu huku uchunguzi ukiendelea.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Babati, Mrakibu wa Polisi Ernesta Mwambinga, alifika eneo la tukio na kuwahakikishia wananchi kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina ili kuwabaini waliohusika na tukio hilo la kinyama.

Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zozote zitakazosaidia uchunguzi, akisisitiza kuwa taarifa hizo zitahifadhiwa kwa siri.

Wananchi wa Magugu wamelalamikia kuongezeka kwa matukio ya ukatili katika eneo hilo, wakitaka ulinzi uimarishwe pamoja na uwekaji wa taa za barabarani, hasa katika maeneo yenye giza nene nyakati za usiku.

Jeshi la Polisi linaendelea na jitihada za kumtambua marehemu na kubaini ukweli wa tukio hilo.

 

Saturday, March 14, 2026

MFUMO WA “ONGEA NA WAZIRI” WAIMARISHA MAWASILIANO KATI YA SERIKALI NA WANANCHI


Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema mfumo wa "Ongea na Waziri" ni daraja muhimu kati ya serikali na wananchi unaolenga kusikiliza moja kwa moja maoni, kero na mapendekezo ya wananchi kuhusu huduma za afya.

Amesema mfumo huo, uliozinduliwa rasmi Januari 26, 2026, unalenga kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma za afya na kuhakikisha maamuzi ya serikali yanaendana na mahitaji halisi ya wananchi.

Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo Machi 13, 2026 wakati wa ziara yake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala jijini Dar es Salaam, ambapo pia alishiriki katika tukio la "Ongea na Waziri" lililowakutanisha watumishi wa afya na wananchi kwa lengo la kusikiliza changamoto na kupokea maoni kuhusu utoaji wa huduma za afya.

Amesema kuanzishwa kwa mfumo huo kunaonesha dhamira ya serikali ya kuweka kipaumbele katika kusikiliza wananchi kama msingi wa kuboresha huduma na kuimarisha uwajibikaji katika sekta ya afya.

Aidha, Waziri Mchengerwa amesema serikali ipo mbioni kuandaa mwongozo utakaotumika katika hospitali zote za serikali ili kukabiliana na malalamiko ya wananchi kuhusu gharama kubwa za matibabu na upatikanaji wa dawa. 


Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, amesema mfumo wa kidijitali wa "Ongea na Waziri" ulioanzishwa na Waziri Mchengerwa unalenga kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika sekta ya afya.

Dkt. Shekalaghe amesema kupitia mfumo huo wananchi wanapata nafasi ya kuwasilisha changamoto na maoni yao moja kwa moja kwa Waziri, jambo linalosaidia kupatikana kwa ufumbuzi wa haraka na kuimarisha utoaji wa huduma za afya.

Ameongeza kuwa wizara itafanya majumuisho ya maswali yaliyoulizwa katika mwezi uliopita ili kutathmini ni maswali mangapi yamepatiwa majibu pamoja na hatua zilizochukuliwa katika kuyatatua.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Mwananyamala, Evancy Asenga, amemshukuru Waziri Mchengerwa kwa ziara yake hospitalini hapo na kuahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa ili kuboresha huduma, hususan katika eneo la mapokezi ya wananchi.

Pia ameomba serikali kufanikisha ujenzi wa jengo kubwa la ghorofa katika hospitali hiyo ili kurahisisha utoaji wa huduma. 


Asenga amesema hospitali hiyo imefanikiwa kufanya mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Dkt. Mercy Maya, amesema hospitali hiyo inaendelea kuimarisha na kupanua huduma za kibingwa kwa kuboresha miundombinu na kuongeza vifaa tiba ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati.

Wednesday, March 11, 2026

WAKAZI MRUKI NA MSASANI WAILILIA SERIKALI DARAJA LA KUDUMU MTO FAHHAY


Na John Walter-Babati

Wakazi wa mitaa ya Mruki na Msasani katika Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani Manyara wameiomba serikali kuwajengea daraja la kudumu katika Mto Fahhay ili kuondoa hatari inayowakabili wanafunzi wa Shule ya Msingi Mruki wanaolazimika kuvuka daraja la mbao kila siku wanapoenda shuleni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi hao wamesema daraja hilo la muda limekuwa likitumika kwa zaidi ya miaka mitatu, lakini kwa sasa limeanza kuwa hatari kutokana na baadhi ya mbao na miti iliyotumika kulijenga kuoza na idadi ya watumiaji kuongezeka.

Shule shikizi ya Msingi Mruki yenye takribani wanafunzi 200 ilianzishwa na Halmashauri ya Mji wa Babati kwa lengo la kupunguza umbali mrefu waliokuwa wakitembea wanafunzi kutoka mitaa ya Mruki na Msasani kwenda katika shule mama ya Msingi Msasani na Darajani.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Msingi Mruki, Bakari Said, amesema licha ya daraja hilo kuwa mkombozi kwa wanafunzi kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu, sasa limekuwa tishio kwa usalama wao hasa wakati wa msimu wa mvua.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mruki, Abdilahi Rajabu, amesema daraja hilo ni kiungo muhimu kinachounganisha mitaa ya Sinai na Mruki, ambapo asilimia kubwa ya watoto kutoka maeneo hayo husoma katika shule hiyo shikizi ya Mruki.

Naye Mariam Hamis, mkazi wa Mruki, ameiomba serikali kuharakisha ujenzi wa daraja la kudumu ili kuwaepusha watoto na wakazi wa eneo hilo na hatari ya kuanguka mtoni wanapovuka.

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo akiwemo Samia Issa Ramadhani na Halima Idd wamesema hulazimika kuvuka daraja hilo kila siku kwenda na kurudi shuleni, hali inayowatia hofu hasa wakati daraja linapokuwa na utelezi au kuharibika.

Aidha, Agostino Balohho, ambaye ni mlinzi wa Shule ya Msingi Mruki, amesema daraja hilo la mbao ni njia fupi inayotumiwa na wanafunzi kutoka Mtaa wa Sinai kufika shuleni na pia hutumiwa na wakazi wa Mruki kama njia ya mkato kwenda mjini Babati kufuata huduma mbalimbali.

Kutokana na hali hiyo, wakazi hao wameiomba serikali pamoja na wadau wa maendeleo kuwasaidia kujenga daraja la kudumu litakalohakikisha usalama wa wanafunzi na wananchi wanaolitumia kila siku.

 


Monday, March 9, 2026

DKT. GWAJIMA AWAHIMIZA WANANCHI KUUPOKEA NA KUULINDA MRADI WA PAMOJA KWA USTAWI WA KIUCHUMI



Na Mwandishi wetu, GEITA

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka wananchi waliopo katika Halmashauri 40 zilizopo katika Mikoa 10 ya Arusha, Mwanza, Kagera, Mara, Singida, Shinyanga, Geita, Rukwa,Tabora na Simiyu waupokee na kuulinda Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia Tanzania (PAMOJA) ili kuwanufaisha wanawake kiuchumi pamoja na kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia (GBV).

Dkt. Gwajima ametoa wito huo  Machi 08, 2026 Mkoani Geita kwa wananchi wa mikoa hiyo 10 na Halmashauri zake 40 ambazo zinatekeleza mradi huo wa PAMOJA, mara baada ya kuuzindua rasmi mradi  wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

"Mradi huu wa PAMOJA wa miaka mitano (5), wananchi na waratibu  mkiupokea,  kuutekeleza na kuulinda ipasavyo, utakuwa ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha wanawake kiuchumi pamoja na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini," amesisitiza Dkt. Gwajima.

Aidha, Waziri Gwajima amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu, kuhakikisha Sekretarieti ya Uratibu wa Mradi wa PAMOJA inaendelea kutimiza wajibu wake kwa weledi na ufanisi ili fursa za mradi ziwafikie na kuwanufaisha walengwa na kumtaka atoe taarifa za mradi kwa umma ili waujue kwani ni mradi uliowalenga wananchi.

Dkt. Gwajima amesema katika kuendeleza azma ya kuwawezesha wanawake kiuchumi, Serikali ya Awamu ya Sita ikiongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inashirikiana na Mdau wa Maendeleo Benki ya Dunia ambayo imetoa mkopo wa  Dola za Marekani Milioni 100 na Ruzuku ya Dola za Kimarekani  Millioni nne (4) sawa na Shilingi Bilioni 262 ili kuwezesha utekelezaji wa mradi huo nchini. 

Mradi huo wa PAMOJA uliozinduliwa na Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima unatekelezwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI  pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto - Zanzibar ambapo utekelezaji wake ulianza rasmi 30 Aprili, 2025 na utafikia tamati Februari 28, 2029.






Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...