Na John walter-Babati
Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Babati limepitisha mapendekezo ya bajeti ya shilingi bilioni 71 kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2026 hadi 2030, ikiwa ni sehemu ya mipango ya kuimarisha utoaji wa huduma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, John Noya, amesema bajeti hiyo inahitaji usimamizi madhubuti na utekelezaji mzuri wa ukusanyaji wa mapato ili iweze kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
"Tusiposimamia vyema mapato yetu, bajeti haitafanya kazi kama ilivyopangwa lakini tukisimamia kwa umakini, itawezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa ufanisi," amesema Noya.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Anna Mbogo amesema kuwa baada ya bajeti hiyo kupitishwa na Bunge, baraza la madiwani kwa kushirikiana na wataalamu wa halmashauri litatoa ushirikiano mkubwa katika hatua za utekelezaji ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda, amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa uwiano wa miradi ya maendeleo katika kata zote, akibainisha kuwa wananchi wote wanastahili kunufaika kwa usawa.
Naye Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Regina Ndege Qwaray, amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, tayari imeanza utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030, hivyo amezitaka halmashauri kuhakikisha mipango yao inaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025–2050.
Amesisitiza kuwa upangaji na utekelezaji wa bajeti za halmashauri unapaswa kulenga maendeleo endelevu yatakayoboresha maisha ya wananchi kwa muda mrefu.