Saturday, May 31, 2025

Simba na Singida mechi ya kisasi nusu fainali CRDB CUP.


Na John Walter -Babati 

Ni kama sinema ya marudio! Baada ya siku chache tu tangu Simba SC waichape Singida Black Stars bao 1-0 kwenye Ligi Kuu ya NBC, timu hizo mbili zinakutana tena kesho, lakini safari hii ni kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB – mechi ya kisasi inayosubiriwa kwa hamu kubwa kwenye uwanja wa Tanzanite, Kwaraa mjini Babati.

Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma, raia wa Kenya, amesema kikosi chake kimejipanga tofauti safari hii na kwamba wamejifunza makosa yao kutoka kwa mechi ya ligi.

"Tunaiheshimu Simba, lakini mechi ya kesho ni hadithi mpya, tupo tayari kupambana na kuhakikisha tunasonga mbele kwenye michuano hii ya CRDB," amesema Ouma.


Kwa upande wa Simba, Kocha Msaidizi Selemani Matola amesema ushindi wa mwisho dhidi ya Singida hauwafanyi wabweteke. "Tunatambua ubora wa Singida Black Stars, ni timu yenye nidhamu ya mchezo, lakini tumejipanga kuhakikisha tunaibuka na ushindi mwingine," amesema Matola.

Nyota wa Simba, Mohamed Hussein maarufu kama "Tshabalala", amesema anajua mchezo utakuwa mgumu lakini wana ari kubwa ya kutetea heshima yao.

"Tunajua haitakuwa rahisi, lakini tumejiandaa kikamilifu," amesema beki huyo kisiki.

Kwa upande mwingine, mshambuliaji wa Singida Black Stars, Eliuter Mpepo, amesisitiza kuwa wameweka msisitizo mkubwa kwenye safu ya ushambuliaji na wana lengo moja tu – kulipiza kisasi. "Tutapambana kwa dakika zote 90, mashabiki wetu waamini tunarudi tofauti kesho," amesema Mpepo.

Mashabiki wa soka mkoani Manyara wanatarajia kushuhudia burudani ya hali ya juu huku uwanja wa Tanzanite ukitarajiwa kufurika mashabiki wanaosubiri kuona nani ataibuka kidedea kwenye mechi hii ya kuvutia.

Je, Simba wataendeleza ubabe wao au Singida Black Stars wataandika historia kwa kulipiza kisasi? Majibu yatapatikana kesho, uwanja wa Tanzanite Kwaraa.
 

Wednesday, May 28, 2025

Waliohitimu kidato cha sita 2025 watakiwa kuripoti kupata mafunzo ya JKT

 


Jeshi la Kujenga Taifa JKT limewataka vijana waliohitimu kidato cha sita mwaka 2025 kutoka shule mbalimbali hapa nchini kujiunga na mafunzo ya jeshi hilo kwa mujibu wa sheria ambapo wanatakiwa kuanza kuripoti kuanzi kesho mei 28, hadi Juni 8 mwaka huu.

Amesema orodha ya vijana ya vijana waliochaguliwa kujiunga na mafunzo hayo inapatikana kwenye tovuti ya JKT ya www.jkt.mil.tz ambapo watapata orodha kamili na mahali walipopangiwa na vitu wanavyotakiwa kuwa navyo wakati wa kujiunga.

Akizungunza na waandishi wa Habari leo Mei 27, 2025 Jijini Dodoma kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT. Meja Jenerali Rajabu Mabele, Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala wa JKT, Kanali Juma Mray amezitaja baadhi ya kambi ambazo vijana hao wanatakiwa kuripoti huku wakiwa na vifaa ni pamoja na vifaa vinavyohitajika.

Kanali Mray amefafanua zaidi ya kuwa kwa vijana wenye ulemavu wa kuona kwa macho wanapaswa kuripoti katika kambi ya ruvu ilioko mkoani pwani kwa ndio kambi yenye miondombinu ya kuwawezesha kupata mafunzo.

Kanali mray amesisitiza kuwa nafasi hizo zinatolewa bure na zinapatikana katika tovuti ambayo imeainishwa na JKT huku akiwasisitiza wanafunzi waliohitimu kidato cha sita mwaka huu na jamii kwa ujumla wasikubali kurubuniwa kuhusu nafasi hizo.

Kanali Mray ametaja baadhi ya vifaa ambavyo wanapaswa kuripoti navyo kuwa ni bukta ya rangi ya 'dark blue' yenye mpira kiunoni(plastic), iliyo na mfuko mmoja nyuma, urefu unaoishia magotini, isiyo na zipu, track suit ya rangi ya kijani au blue, nataka zote zinazohitajika katika udahili wa kujiunga na elimu ya juu, zikiwemo cheti cha kuzaliwa,.

Amesema ili kufahamu kambi ambayo kijana aliyopangiwa atatakiwa kuingiza jina la shule au namba ya shule aliyohitimu elimu ya kidato cha sita ndipo atapata orodha kamili ya majina hayo.

Wednesday, May 21, 2025

DKT. KILABUKO AZINDUA MWONGOZO WA KITAIFA KWA WATOA HUDUMA ZA MAENDELEO YA BIASHARA


NA. MWANDISHI WETU - DAR ES SALAAM

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. James Kilabuko amezindua rasmi Mwongozo wa Kitaifa kwa Watoa Huduma za Maendeleo ya Biashara katika hafla iliyofanyika kwenye Hoteli ya Four Points by Sheraton, Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza hii leo tarehe 21 Mei 2025 wakati wa uzinduzi  huo kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi, Naibu Katibu Mkuu huyo amesema kuwa Mwongozo huo unaweka msingi wa mabadiliko makubwa ambayo yatawawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara wakubwa kukuza biashara zao na kuchangia kikamilifu kwenye uchumi wa Taifa.

"Uwepo wa Mwongozo huo unalenga kuweka viwango, mwelekeo na uratibu wa huduma zinazotolewa kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini, hivyo umekuja kwa wakati sahihi na tunaamini utaleta matokeo chanya kama ilivyokusudiwa," alisema Dkt. Kilabuko.

Aidha alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada anazozifanya katika kuhakikisha mazingira ya wafanyabiashara na wawekezaji nchini yanaendelea kuwa bora.

"Kwa umuhimu wa pekee napenda kumshukuru kwa dhati, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada anazofanya katika kufungua uchumi na kuchochea biashara na uwekezaji nchini.Rais wetu ameboresha mazingira ya biashara nchini na kuchochea kuanzishwa kwa shughuli za kiuchumi nyingi katika sekta mbalimbali. Shughuli hizo pia zinahitaji huduma za maendeleo ya biashara ili kuwa shindani. 

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wanamanchi Kiuchumi (NEEC) Bi. Beng'i Issa ameleeza kuwa Mwongozo wa Huduma za Maendeleo ya Biashara kwa Watoa Huduma za Maendeleo ya Biashara Tanzania unalenga kuboresha utoaji wa huduma za biashara ikiwa ni pamoja na: ushauri, mafunzo, msaada wa kiufundi, ujuzi, uatamizi, uhusiano baina ya wafanyabiashara, mawasiliano, na usimamizi wa biashara.

"Tunategemea, Mwongozo huu unakwenda kutoa dira ya namna bora ya utoaji wa huduma za biashara Tanzania zinazoweza kuboresha biashara na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujuml," alisema Bibi. Beng'i.

Alifafanua kuwa, mwongozo huo utaleta matokeo chanya na kuwasihi watoa huduma za maendeleo ya biashara nchini kutumia Mwongozo huu kama nyenzo katika kuwahudumia wafanyabiashara wadogo na wa kati wanaotekeleza shughuli za kiuchumi katika sekta mbalimbali. 

Naye Balozi wa Canada nchini Tanzania, Mhe. Emily Burns, amepongeza jitihada hizo za kuhakikisha mwongozo unazinduliwa huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kadiri inavyotakiwa na kueleza kuwa wanathamini uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina yao na Tanzania na wataendelea kushiriki katika masuala mbalimbali ikiwemo  kuunga mkono sekta ya afya, elimu, biashara na uwekezaji, kilimo, ulinzi na usalama. 
 
Akizungumzia umuhimu wa mwongozo huo Mkurugenzi mkazi wa MEDA Musa Lugambo amesema kuwa mwongozo huo utawasaidia sana watoa huduma kuweza kuwasaidia kutoa huduma ambayo itawasaidia wajawasiriamali kwa ajili ya kutekeleza biashara zao. 

"Tumekuwa na changamoto kwa watoa huduma ambapo unakuta kwamba huduma ambayo inayotolewa kwa wajawasiriamali inakuwa siyo ya kiwango kizuri na hivyo kushindwa kuwasaidia wajawasiriamali kuendeleza biashara zao" Amesema Lugambo

AWALI
Uzinduzi huo umeratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) na kusimamia zoezi la uandaaji wa Mwongozo wa Kitaifa kwa Watoa Huduma za Maendeleo ya Biashara kwa udhamini wa MEDA. Aidha umehudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka Serikalini, sekta binafsi, taasisi za fedha na watoa huduma wa maendeleo ya biashara na kujumuisha matukio mbalimbali ikiwemo hotuba za viongozi, majadiliano ya kitaalamu na maonesho ya huduma kutoka kwa taasisi shiriki.



Source

Video Mpya : KACHOJI - CHANGAMOTO

 

Wawili wahukumiwa miaka 20 jela kwa kukutwa na nyara ya serikali.



Na John Walter -Babati 

Mahakama ya Wilaya ya Babati leo Mei 20, 2025 imetoa hukumu ya kifungo cha miaka 20 jela kwa wanaume wawili waliopatikana na hatia ya kumuua pundamilia na kumiliki nyara za serikali kinyume cha sheria.

Washtakiwa hao ni Ramadhan Hussein Dodi (39) na Mohamed Bakari Chora (30), wakazi wa Kijiji cha Chubi, Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma. Walipatikana na hatia ya kutenda kosa hilo mnamo Oktoba 25, 2024 katika eneo la Chubi lililopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Wilaya ya Babati mkoani Manyara.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyosomwa mahakamani, washtakiwa walikamatwa wakiwa na kichwa cha pundamilia, miguu ya pundamilia, mkia mmoja pamoja na ngozi ya mnyama huyo. Nyama ya pundamilia waliokuwa wakimiliki ilikadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Kimarekani 1,200, sawa na takribani shilingi milioni 3,204,000 za Kitanzania.

Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati, Mheshimiwa Karimu Mushi (PRM), ambapo wote wawili walitiwa hatiani na kuhukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja.

Makosa hayo ni kwa mujibu wa kifungu cha 86 (1) na (2)(c)(iii) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori, Sura ya 283 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, pamoja na Aya ya 14, Kifungu namba 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Kuhujumu Uchumi, Sura ya 200 iliyofanyiwa marejeo mwaka huohuo.

Mwendesha mashtaka wa serikali alikuwa Bw. Rusticus Mahundi, huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Simon Shirima.

Ingawa wamepatikana na hatia, washtakiwa wamepewa haki ya kisheria ya kukata rufaa endapo hawajaridhika na uamuzi wa mahakama.

Hukumu hiyo imetajwa kuwa onyo kwa wale wote wanaojihusisha na ujangili na uharibifu wa rasilimali za taifa, hasa wanyamapori walio katika hatari ya kutoweka. 

Tuesday, May 20, 2025

WIKI YA MAZIWA 2025 KUADHIMISHWA MKOANI MOROGORO


KUELEKEA Kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Maziwa mwaka huu, Bodi ya Maziwa nchini imeendelea kutoa wito kwa wananchi kuongeza unywaji wa maziwa, hasa yale yaliyosindikwa, ili kuboresha afya, lishe bora na kuunga mkono sekta ya maziwa nchini.

Akizungumza na waandishi wahabari leo Mei20,2025 katika mafunzo yaliyotolewa jijini Dar es salaam, Kaimu Msajili Bodi ya maziwa Tanzania Deorinidei Mng'ong'o amesema maziwa yaliyosindikwa ni salama kwa matumizi ya binadamu, yanadumu kwa muda mrefu na yana viwango bora vya usafi na virutubisho, hivyo kuwa chaguo bora kwa jamii zote, mijini na vijijini.

"Tunapoelekea kilele cha Wiki ya Maziwa, tunawakumbusha wananchi kuwa kuchagua maziwa yaliyosindikwa si tu ni njia ya kulinda afya zao, bali pia ni kuunga mkono juhudi za wakulima na viwanda vya maziwa nchini," alisema Kaimu Msajili wa Bodi hiyo.

Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa maziwa katika lishe, kuhamasisha matumizi yake, na kutoa fursa kwa wadau wa sekta hiyo kuonesha mafanikio na changamoto zinazowakabili.

Maadhimisho ya mwaka huu yanatarajiwa kufanyika mkoani Morogoro kuanzia mei 27 hadi juni mosi mwaka huu.

Bodi ya Maziwa imeandaa shughuli mbalimbali zitakazofanyika kuelekea na wakati wa kilele cha wiki hiyo, zikiwemo maonesho ya bidhaa za maziwa, midahalo ya kitaaluma, na kampeni za uelimishaji mashuleni na katika jamii kwa ujumla.

SIKU YA VIPIMO DUNIANI, WADAU WAHIMIZWA KUFUATA VIWANGO VYA KIMATAIFA


Farida Mangube, Morogoro

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, ametoa wito kwa wananchi na taasisi zote kuhakikisha wanazingatia ubora wa vipimo katika shughuli zao za kila siku, akisisitiza kuwa vipimo visivyo sahihi vinaweza kuathiri afya, usalama, haki katika biashara, na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

DC Kilakala alitoa kauli hiyo Mei 20, kwenye Maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Morogoro, ambapo amsema vipimo sahihi ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisayansi. 

"Tunapoadhimisha Siku ya Vipimo Duniani, ni wajibu wetu kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika shughuli zetu za kila siku vinakidhi viwango vya kimataifa."

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, amesema kuwa uhakiki wa usahihi wa vipimo katika sekta kama viwanda, afya, ujenzi, na usafiri wa anga ni hatua muhimu ya kuhakikisha bidhaa na huduma zinazotolewa zina ubora unaostahili na zinawalinda watumiaji.

"Vipimo vikihakikiwa kwa usahihi wake vitaleta manufaa makubwa kwa jamii," alisema Dkt. Katunzi. 

"Vitawezesha utoaji wa huduma bora na bidhaa zenye ubora katika sekta kama afya, mawasiliano, chakula, na nyingine nyingi."

Aidha, amesema Tanzania, kupitia maabara ya TBS, imekuwa nchi ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki kupata ithibati ya kimataifa katika vipimo vya torque, barometa na unyevu — hatua inayoiwezesha kutoa huduma za ulinganifu wa vipimo kwa kiwango cha kimataifa.

Katika maadhimisho hayo TBS imewakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali za umma na binafsi ambapo Kaulimbiu ya mwaka huu ni "Vipimo kwa Nyakati Zote na kwa Watu Wote", ikisisitiza umuhimu wa vipimo sahihi katika kuchangia maendeleo endelevu na ustawi wa jamii katika nyanja zote za maisha.

Monday, May 19, 2025

WANAFUNZI WA CHIKUKWE WAMSHUKURU RAIS SAMIA KWA MADARASA MAPYA

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Ismail Ally Ussi akiweka jiwe la msingi katika shule ya msingi Chikukwe wilayani Masasi Mkoa wa Mtwara
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Ismail Ally Ussi akizungumza baada ya kufika katika Shule ya Msingi Chikukwe iliyopo Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara kabla ya kuweka jiwe la msingi katika shule hiyo

Shule iliyowekwa jiwe la msingi Chikukwe na Mwenge wa Uhuru Wilayani Masasi

Na Regina Ndumbaro Masasi-Mtwara 

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Chikukwe iliyopo katika Wilaya ya Masasi wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia madarasa mawili mapya. 

Shukrani hizo zimetolewa mara baada ya Mwenge wa Uhuru kuweka jiwe la msingi katika madarasa hayo mapya, hafla iliyoongozwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025, Ndg. Ismail Ally Ussi.

Katika hafla hiyo, Ndg. Ussi ameitaka jamii kushiriki kikamilifu katika kutunza miundombinu ya shule hiyo kwa ajili ya manufaa ya sasa na vizazi vijavyo. 

Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya wananchi na serikali ni msingi imara wa maendeleo ya sekta ya elimu nchini.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetumia kiasi cha shilingi 66,330,000 kukamilisha ujenzi wa madarasa mawili ya wanafunzi wa awali pamoja na ujenzi wa matundu sita ya vyoo katika shule hiyo. 

Ujenzi huo unalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wa shule ya awali.

Mwenge wa Uhuru umekamilisha mbio zake katika halmashauri mbili za Wilaya ya Masasi ambazo ni Masasi TC na Masasi DC, ambapo miradi mbalimbali imetembelewa, kukaguliwa na kuonwa. 

Ifikapo tarehe 20 Mei 2026, Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuelekea Halmashauri ya Wilaya ya Newala kuendelea na mbio zake.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...